Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeushauri Uongozi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA) kupeleka ubunifu wa bidhaa unaotakana na wanafunzi na wakufunzi kwa wananchi ili kuchangia kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii.
Wameyasema hayo Machi 16, 2023 walipotembelea kukagua shughuli mbalimbali zinazoendeshwa chuoni hapo huku wakitolea mfano ubunifu wa umwagiliaji uliopo chuoni hapo.
Kamati pia imeutaka uongozi wa chuo kukiendesha chuo kwa kufuata misingi na maadili ili kumuenzi Baba wa Taifa ambaye chuo hicho kimebeba jina lake.
"Kumekuwa na mmomonyoko mkubwa wa maadili kwa vijana wengi hapa nchini shule na vyuoni, chuo hiki kimebeba jina la mtu mashuhuri anayeheshimika na Taifa hadi leo hivyo kinatakiwa kimuakisi mhusika," amesema Mhe. Dkt Thea Ntara, Mbunge anaewakilisha Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu.
Kamati pia imekipongeza Chuo hicho kwa kutumia mapato yake ya ndani kufanya maboresho ikiwemo ujenzi wa maktaba na ukumbi mpya wa mihadhara ambao mpaka sasa umefikia asilimia 25.
Kwa upande wake Prof. Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ameahidi kufanyia kazi maoni na mapendekezo ikiwemo kuandaa taarifa ya kuelezea ubunifu unaofanyika umefikia hatua gani.
Amesema ubunifu hauishii ndani ya vyuo tu bali hufikia hatua ya kubiasharishwa na Serikali imekuwa ikiwasaidia wabunifu kufikia hatua hiyo.
Awali akitoa taarifa ya chuo, Mkuu wa MNMA Prof. Shadrack Mwakalila amesema ili kukidhi mahitaji ya ongezeko la wanafunzi, katika mwaka 2021/22 chuo kilianzisha ujenzi wa jengo lenye maktaba na ukumbi wa mihadhara kwa kutumia mapato ya ndani.
Amesema ujenzi huo unatarajia kugharimu zaidi ya Shilingi bilioni 15.5 na kuwa maktaba itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 2,500 kwa wakati mmoja na ukumbi wa mihadhara wanafunzi 1,000.


