KAMATI ya kudumu ya Bunge ya afya na masuala ya UKIMWI imeimwagia sifa Serikali ya Rais Samia kwa kutekeleza mradi wa jengo la huduma ya afya ya mama na mtoto uliogharimu zaidi Bilioni 12 katika hospitali ya Rufaa ya kanda - Mbeya.
Akiongea kwa niaba ya kamati hiyo leo Machi 16, 2023 Mwenyekiti wa kamati Mhe. Stanslaus Nyongo amesema tumetembelea maeneo mengi hatujawai kuona jengo zuri lililojengwa kisasa kama jengo hili la mama na mtoto lilojengwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya.
"Tumeona maeneo mbalimbali ambayo yamejengwa kwa ustadi wa juu, pamoja na wodi za kisasa kabisa kwaajili ya viongozi na watu wenye uwezo fedha za kutosha, hivyo ujenzi huu umekidhi mahitaji makubwa na hii kwa sisi Tanzania tunajivunia kwakweli kwa ukanda wa Afrika tunaingia katika utoaji huduma katika kiwango cha juu." Amesema.
Aidha Mhe. Nyongo Aidha, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa katika kuelekea kipindi cha miaka miwili madarakani kwa jitihada zilizofanywa katika kufanikisha wa ujenzi wa mradi huo ambao ni wa ghorofa sita wenye uwezo wa kuchukua Takribani wagonjwa 200.
Nae, Dkt. Godlove Mbwanji, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya amesema matarijio yao kufikia tarehe 30 aprili, 2023 huduma katika jengo hilo zitaanza kupatikana kwa 100 % japo kwasasa baadhi ya huduma zinaendelea kulingana na viendea kazi vilivyopo.

