UBALOZI WA TANZANIA NCHINI CHINA WAANZISHA PROGRAMU YA KUWASAIDIA WAFANYABIASHARA WA KITANZANIA.

MUUNGANO   MEDIA
0

 


Na Mwandishi Wetu - Beijing, China

Ubalozi wa Tanzania nchini China umeanzisha programu ya elimu kwa umma kuwasaidia Watanzania kununua mashine mbalimbali kwa bei nafuu nchini humo.

Hayo yameelezwa na Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki ofisini kwake Beijing, China alipokutana na Watanzania ambao wapo nchini humo kwa mafunzo ya muda mfupi ya kujifunza namna China ilivyojiondoa katika umasikini kwa kipindi kifupi pamoja na fursa mbalimbali zinazopatikana nchini humo.

"Tumeanzisha programu ya kuwawezesha Watanzania kupata taarifa ya mashine zinazopatikana China kwa gharama nafuu  ili kuongeza thamani ya mazao yanayolimwa Tanzania. Mfano kuna mashine kwa ajili ya zao la Alizeti ambayo inauzwa Dola za Kimarekani 300, ambayo kama mtu atainunua ataweza kutengeneza mafuta ya Alizeti ambayo yatakuwa yameongezwa thamani," amesema Balozi Kairuki.

Ameendelea kusema kuwa, ni wakati sasa wa vijana kujielekeza katika masuala ya viwanda vidogi ili kuinua uchumi wao, ambapo kwa kununua mashine moja inaweza kumuondoa kijana katika utegemezi wa wazazi, ndugu au kusubiri ajira.

"Kuna mashine ya kupiga lipu ambayo inauzwa dola 1,000 ukiwa nayo unaweza kukodisha kwa mafundi ujenzi kwa shilingi 400,000 kwa siku. Kwa hiyo, badala ya kijana kutumia fedha nyingi kununua simu ya gharama, anaweza kutumia fedha hizo  kununua mashine ambayo itamwingizia fedha na kutokuwa tegemezi kwa wazazi, walezi au kusubiri ajira," amefafanua Balozi Kairuki.

Vilevile Balozi Kairuki ametoa rai kwa Watanzania kutumia Ubalozi huo kupata taarifa za makampuni au watu wanaofanya nao biashara kabla ya kufanya malipo yoyote ili kuepuka utapeli.

"Tunashauri Wafanyabiashara wa Kitanzania kabla ya kufanya malipo yoyote wawasiliane na ubalozi, ili tufuatilie kama kweli kampuni unayotaka kufanya nayo biashara kweli ipo na inauza bidhaa unazohitaji. Ukitupa taarifa baada ya kutapeliwa inakuwa ngumu kufuatilia sababu China ni kubwa na ina watu wengi sana. Hivyo ni vizuri kupata taarifa ya kampuni husika kabla ya malipo," amesema Balozi Kairuki.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)