NCHI ZA SADC ZAWEKA MIKAKATI YA KUJIKWAMUA KIUCHUMI.

MUUNGANO   MEDIA
0

Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umehitimidhwa jijini Kinshasa tarehe 19 Machi 2023, huku agenda za kujikwamua kiuchumi katika kanda hiyo ya Kusini mwa Afrika zikipewa kipaumbele.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unaotathmini utekelezaji wa mipango ya Mwaka wa Fedha 2022/2023 na kuweka mikakati ya utekelezaji wa mipango ya Mwaka wa Fedha 2023/2024, umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb) akisaidiana na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde (Mb).

Maeneo ambayo Mhe. Waziri Tax alichangia wakati taarifa za utekeleaji zilipokuwa zinawasilishwa ni pamoja na hatua iliyofikiwa kuhusu tafsiri ya nyaraka muhimu za SADC katika lugha ya Kiswahili, ujenzi wa Sanamu la Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Mpango wa Kanda wa ununuzi wa pamoja wa vifaa vya afya unaoratibiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Mhe. Waziri Tax alisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi katika utekelezaji wa maeneo hayo, kufuatia maelezo kuwa utekelezaji wa tafsiri ya nyaraka muhimu za SADC katika lugha ya Kiswahili upo katika hatua za kumpata mzabuni wa kufanya kazi hiyo na ujenzi wa Sanamu la Baba wa Taifa unaendelea, na kazi hiyo inatakiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2023. Kuhusu Mpango wa Kanda wa ununuzi wa pamoja wa vifaa vya afya, Dkt. Tax alisema MSD inaendelea na jukumu hilo na kutoa wito kwa nchi wanachama kuongeza kasi ya kuitumia bohari hiyo ya dawa kwa kuwa manufaa yake ni makubwa hususan katika kupunguza gharama za ununuzi wa dawa na vifaa tiba.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)