NYUMBA 196 ZILIZOJENGWA NA WHI JIJINI DODOMA ZAIKOSHA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA.

MUUNGANO   MEDIA
0

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama amesema kamati yake imeridhishwa na viwango vya nyumba 196 zilizojengewa na Watumishi Housing Investments (WHI) kwa kuzingatia kipato cha watumishi wa umma ili wapate makazi bora yatakayowawezesha kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mhe. Dkt. Mhagama amesema hayo, wakati wa ziara ya kikazi ya Kamati yake ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa nyumba 196 zilizojengwa na Watumishi Housing Investments (WHI) eneo la Njedengwa jijini Dodoma, lengo likiwa ni kujiridhisha na utekelezaji wa bajeti iliyotegwa na Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/23 kuiwezesha WHI kutekeleza mradi huo.

Mhe. Dkt. Mhagama amefafanua kuwa, lengo kubwa la utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa nyumba katika eneo la Njedengwa jijini Dodoma ni kuwawezesha watumishi wa umma kupata nyumba za bei nafuu ili waweze kuwahudumia Watanzania kwa ufanisi zaidi.

Mhe. Dkt. Mhagama amesema, kamati yake imeridhishwa na hatua ya kukamilika kwa nyumba 196 katika kipindi cha muda mfupi na imefurahishwa na mwitikio wa watumishi wa umma kuzichangamkia nyumba hizo ambapo asilimia 94 ya nyumba hizo zimeshapata wanunuzi.

“Kitendo cha asilimia 94 ya nyumba 196 zilizojengwa WHI kupata wanunuzi kinaonyesha kuwa ujenzi wa nyumba hizo umezingatia hali halisi ya kipato na mahitaji ya watumishi wa umma na kuongeza kuwa, Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anastahili kupongezwa kwa kuwezesha utekelezaji wa mradi huo,” Mhe. Dkt. Mhagama amesisitiza.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema, amekuwa akiisisitiza WHI kujenga nyumba za gharama nafuu kwa ajili ya watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuwawezesha kupata makazi bora ya kuishi.

Mhe. Jenista Mhagama amesema, ataendelea kuisisitiza WHI kujenga nyumba za gharama nafuu kwa ajili ya watumishi wa umma nchini kwani ujenzi wake unapaswa kuhakikisha bei ya nyumba hizo unazingatia kipato cha watumishi wa umma kama ilivyoelekezwa na Mhe. Rais

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)