Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Anthony Mavunde aitaka Taasisi ya Uthibiti na Udhibiti wa Mbegu Tanzania (TOSCI) kuhakikisha inaweka mkazo mkubwa kwenye ukaguzi wa mashamba ya mbegu ili kuhakikisha mbegu zinazosambazwa kwa wakulima kuwa ni mbegu bora na zitakazosaidia uzalishaji wa tija.
Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo leo tarehe 15 Machi, 2023 alipotembelea na kukagua utekelezaji wa majukumu wa TOSCI.
"Mbegu ni tasnia muhimu sana, hatutaweza kujitosheleza kwa chakula au kufikia malengo tuliyojiwekea katika uzalishaji wa mazao pasipo kuwa na uhakika wa mbegu bora. Serikali yenu inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuongeza uwekezaji kwenye utafiti na uzalishaji wa mbegu bora nchini ili tuweze kufikia malengo makuu ya kukuza kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.
Ni lazima TOSCI mtimize jukumu hili lenu kubwa la kuhakisha mashamba ya uzalishaji ya mbegu yanakaguliwa,kwasababu ninyi ndio wenye dhamana ya uthibiti na udhibiti wa mbegu hapa nchini.Rai yangu kwenu ni kuimarisha ukaguzi ili mkulima apate anufaike na mbegu bora.
Serikali itahakikisha inaendelea kuwekeza katika vifaa na miundombinu bora ili kurahisisha jukumu lenu hili sambamba na kuwajengea uwezo watumishi wa TOSCI ili waweze kutekeleza majukumu yao kiufanisi kwa kufuata misingi ya utaalamu wa kazi yao, kwani wanachofanya kina manufaa makubwa sana kwa wakulima na nchi kwa ujumla.
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo itaendelea kutafuta fursa mbalimbali nje ya nchi na kuwawezesha wataalam wengi zaidi wa TOSCI kwenda kujifunza ili kuleta manufaa zaidi kwa tasnia ya mbegu na Taifa kwa ujumla.
Ninawapongeza sana kwa kazi kubwa ya maboresho ya maabara na ujenzi wa maktaba,ni imani yangu kwamba hatua hii itaongeza zaidi ufanisi katika kutekeleza majukumu yenu”Alisema Mavunde.


