Na WyEST, MOROGORO.
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeshauriwa kuendelea kukiwezesha Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwenye eneo la utafiti ili kuweza kufikia malengo waliyojiwekea.
Hayo yamesemwa Machi 15, 2023 Mkoani Morogoro na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo Mhe. Dkt. Kitila Mkumbo wakati Kamati hiyo ilipotembelea kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa chuoni hapo.
Kamati imeelekeza pia chuo hicho kuendelea kujitangaza zaidi kutokana na kuwepo na vitu vingi vizuri ambavyo wananchi wengi wangependa kuvifahamu.
"Chuo hiki kina mambo mengi sana mazuri ambayo wadau wangependa kuyafahamu kwa undani hivyo ni vema mngezitangaza shughuli zilizopo hapa ili wadau waweze kuzifahamu," amesema Dkt. Mkumbo.
Aidha Kamati hiyo imeelezea kuridhishwa kwake na shughuli zinazotekelezwa katika chuo hicho na kuahidi kuendelea kutoa maoni ya kuendelea kukiboresha zaidi.
Naye Mhe. Omari Kipanga, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ameshukuru Kamati kwa kutembelea chuo hicho na kuahidi kufanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati hiyo.
"Tunashukuru kwa kutembelea chuo chetu na tunaahidi kufanyia kazi maoni na mapendekezo yote mliyotoa ili kuendelea kuboresha chuo," amesema Mhe. Kipanga.
Awali akitoa taarifa ya chuo, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda amesema kina jumla ya ndaki (colleges) saba ambazo ni kilimo, misitu, wanyamapori na utalii, tiba ya wanyama na sayansi za afya, sayansi za jamii na insia, uchumi na stadi za biashara, elimu na sayansi na kampasi ya Mizengo Pinda.
Ameongeza kuwa katika nyanja ya utafiti SUA imeendelea kufanya vizuri kwa kushika nafasi ya kwanza kitaifa na ya 42 katika bara la Afrika katika matokeo yaliyotolewa na Google Scholar Citation Index Julai 2022.
"Aidha katika watafiti bora 1,000 nchini, SUA imetoa watafiti 222 na kati ya watafiti bora 100 nchini SUA ilitoa 33 na mtafiti bora namba moja nchini pia ametokea SUA," ameongeza Prof. Chibunda.



