Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kujenga ofisi Makao Makuu ya nchi Dodoma ambayo itaiwezesha taasisi hiyo kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa nchini.
Mhe. Dkt. Mhagama ametoa pongezi hizo wakati wa ziara ya kikazi ya Kamati yake ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa ofisi ya makao makuu ya TAKUKURU jijini Dodoma, kwa lengo la kujiridhisha na utekelezaji wa bajeti iliyotegwa na Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/23 ili kuiwezesha TAKUKURU kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Mhe. Dkt. Mhagama amesema, kwa ujumla kamati yake inampongeza sana Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ametoa kipaumbele cha kuziwezesha taasisi zote zinazotoa haki nchini ikiwemo TAKUKURU ambayo imepatiwa fedha kujenga jengo la makao makuu ya taasisi hiyo jijini Dodoma.
Mhe. Dkt. Mhagama ameongeza kuwa, mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa ndio yataiwezesha nchi kufikia malengo ya maendeleo hivyo, mradi wa ujenzi wa ofisi ya TAKUKURU makao makuu ukikamilika kwa wakati utaiwezesha taasisi hiyo kutekeleza jukumu lake la msingi la kuzuia vitendo vya rushwa nchini.
“Sisi kama kamati tunatambua mchango na kazi kubwa anayoifanya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa akisadiwa na Mhe. Jenista Mhagama pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU CP Salum Hamduni,” Dkt. Mhagama amesisitiza.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema jengo hilo la ofisi ya makao makuu ya TAKUKURU jijini Dodoma linajengwa kwa kuzingatia majukumu yanayotekelezwa na TAKUKURU kwa mujibu wa Sheria.
Mhe. Jenista Mhagama ameongeza kuwa, katika jengo hilo, mifumo yote muhimu ya TEHAMA imewekwa kuiwezesha taasisi hiyo kufanya kazi kisasa na kukidhi viwango vya kimataifa.

