Na.Elimu ya Afya kwa Umma.
Ubunifu uliofanywa na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando mkoani Mwanza wa kumtibu majeruhi aliyejeruhiwa na moto kwa kutumia majani ya migomba umemfurahisha Naibu Waziri wa Afya Dkt.Godwin Mollel na kuagiza ubunifu huo uendelezwe na kuweza kutumiwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini .
Dkt.Mollel ametoa maagizo hayo Machi 19.2023 Jijini Dodoma katika Maadhimisho ya Miaka 70 ya Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania yanayokwenda sambamba kaulimbiu isemayo”Bima ya Afya kwa Wote Muuguzi na Mkunga Tarajio la Huduma Bora’’.
Dkt.Mollel amesema Hospitali ya Rufaa Bugando imefanya juhudi kubwa kuhakikisha inafanya ubunifu huo wa kutumia majani ya migomba kutoa huduma kwa mtu aliyeungua moto .
“Mlichofanya Bugando ni kitu kizuri sana, hivyo aliyefanya ubunifu huu wa kutumia majani ya mgomba kumhudumia mtu aliyeungua moto lazima anufaike kutokana na ubunifu wake hivyo ni ,muhimu kuwezeshwa na kuendeleza na kuutumia ubunifu huu katika maeneo mbalimbali”amesisitiza Dkt.Mollel.
Aidha, Dkt.Mollel amesema Elimu ya Afya kwa umma kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Bugando ni wakati wake sahihi wa kuielimisha jamii umuhimu wa kuyatumia majani ya migomba katika kumhudumia mtu aliyeungua moto ili kurejesha ngozi yake katika hali ya kawaida kwa gharama nafuu .
“Elimu ya Afya kwa Umma ni wakati wenu kuelimisha jamii namna majani haya jinsi yanavyoweza kurecover ngozi ya mtu iliyoungua na kurejea katika hali yake ya kawaida , pia waandishi wa habari ni muhimu kutumia kalamu zenu kuipa uelewa jamii kuhusu majani haya ya migomba”amesema.
Kwa upande wake Afisa Muuguzi Kiongozi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando Stellarodia Ndyamkama amesema ubunifu wa kutunza vidonda kwa kutumia majani ya migomba kwani pamekuwa na faida kubwa ikiwemo vidonda kupona kwa uharaka.
“Panapokuwepo majani ya migomba kwenye kidonda hakuna uwezekano wa kupata mashambulizi ya wadudu wengine ama maambukizi na kidonda kinapofunikwa kwa jani la mgomba hakivimbi sana kinakuwa katika hali ya kawaida ,na kijani kilichopo katika jani la ,mgomba kinasaidia kutokuwa na harufu mbaya ,faida nyingine mgonjwa anapunguza maumivu ndani ya mgomba na damu haitoki ovyo ndani ya kidonda,unyevunyevu unarahisisha kupona haraka “amesema.
Aidha,Ndyamkama amesema jani la mgomba linasaidia kulinda joto la mwili huku akitumia fursa hiyo kumshukuru Naibu Waziri wa Afya Dkt.Godwin Mollel kwa kulipokea suala hilo kwa mitazamo chanya katika kuwapunguzia wananchi gharama za matibabu .
Kuhusu ushirikiano na Elimu ya Afya kwa Umma Ndyamkama amesema Hospitali ya Bugando Kitengo cha Wagonjwa waliopata ajali za moto wapo tayari kwa ushirikiano utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu njia hiyo ya kutumia majani ya mgomba.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Dkt.Godwin Mollel amesema ni vyema Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kumtumia Muuguzi kutoka Zahanati ya Wellu Halmashauri ya Mbozi Joel katika masuala mbalimbali ya uelimishaji kwa kutumia sanaa yake ya uimbaji ambapo Naibu Waziri ameahidi kumpatia Tsh.milioni mbili baada ya kutunga wimbo mzuri katika maadhimisho ya miaka 70 ya Uuguzi na Ukunga.
Pia, Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amezindua mfumo wa kuhifadhi taarifa za Wauguzi na Wakunga utakao wezesha kupata taarifa zao kwa wepesi.
