WAUGUZI NA WAKUNGA WANA MCHANGO MKUBWA KUOKOA UHAI WA WATU-DKT.MOLLEL.

MUUNGANO   MEDIA
0

Na.Elimu ya Afya kwa Umma.

Naibu Waziri wa Afya Dkt.Godwin Mollel amewataka watumishi kada ya afya hususan Wauguzi na Wakunga kuendelea kufuata taratibu na sheria ili kuweza kuendelea kutoa huduma bora za afya kwani wana mchango mkubwa katika kuokoa uhai wa watu.   

Dkt.Mollel amebainisha hayo Jijini Dodoma katika Maadhimisho ya Miaka 70 ya Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania yanayokwenda sambamba kaulimbiu isemayo”Bima ya Afya kwa Wote Muuguzi na Mkunga Tarajio la Huduma Bora’’.

“Tunapozungumzia afya ni kulinda uhai wa binadamu , katika viungo vital ambavyo ni muhimu sana ni Manesi tuwape kipaumbele ili kuokoa uhai wa watu kwani wao huonana mara kwa mara na wagonjwa “amesema Dkt.Mollel.

Aidha, Dkt.Mollel amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa Tsh.bilioni 51.8 katika kada ya afya, na Tsh.bilioni 54.2 kwa ajili ya Hospitali za Mikoa huku Tsh.bilioni 290 kwa ajili ya Vifaa Tiba.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya,Dkt.Seif Shekalaghe, Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya Ziada Sellah amesema elimu na huduma mbalimbali za afya ikiwemo uelewa juu ya afya ya akili,huduma za macho na kuchangia damu zimetolewa katika maadhimisho hayo.

Kwa upande wake Mwenyekiti Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania Prof. Lilian Mselle amesema ajenda ya Wauguzi ni kujielekeza zaidi kwenye ubora wa huduma katika kuelekea Bima ya Afya kwa Wote na kuweza kupunguza vifo vya mama na mtoto huku lengo la baraza hilo ni kusimamia taaluma ya Wauguzi na Wakunga na kushirikiana na Wizara ya Afya katika utoaji wa elimu ya afya dhidi ya maradhi.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)