Na. Elimu ya Afya kwa Umma.
Msingi wa afya njema ni Lishe bora inayotokana na kula mlo kamili wakati wote. Mlo kamili ni ule ambao hutokana na chakula mchanganyiko kutoka katika makundi yote ya chakula. Mlo kamili huupatia mwili virutubishi (viini lishe) vyote muhimu unaohitaji kwa ajili ya afya bora. Ni muhimu kula chakula mchanganyiko (mlo kamili) katika kila mlo kwa sababu hakuna chakula chochote kinachoweza kutosheleza mahitaji ya virutubishi mwilini kwani vyakula hutofautiana aina, kiasi/wingi na ubora wa virutubishi.
Hayo yamebainishwa na Afisa Lishe wa Wilaya ya Bagamoyo, Bi. Sophia Makame; wakati akitoa elimu ya jinsi ya kuandaa mlo kamili kwa wanawake 42 wa dini ya Kiislaam wa msikiti wa Wazee kata ya Magomeni, Halmashauri ya Bagamoyo Mkoani Pwani mnamo tarehe 17.03.2023.
Bi Sophia alieleza jinsi ya kupanga mlo kamili; "mlo kamili hupangwa kwa kuchagua angalau chakula kimoja kutoka katika kila kundi la chakula, na huandaliwa kwa urahisi kwa kutumia vyakula vinavyopatikana katika mazingira tunayoishi"
"Makundi ya chakula ni mgawanyo wa vyakula kulingana na virutubishi/viini lishe katika vyakula hivyo" alisema.
Bi. Sophia alibainisha makundi hayo ya chakula ambayo ni:
i. Vyakula vya nafaka, mizizi na ndizi za kupika
ii. Vyakula ya jamii ya mikunde na vyenye asili ya wanyama
iii. Matunda
iv. Mbogamboga
v. Sukari, Asali na Mafuta
Bi. Sophia alihimiza kuandaa mlo kamili wakati wote wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan ili kuweza kutosheleza mahitaji ya virutubishi mwilini kwao na wanafamilia wote.
Bi. Sophia alihitimisha kwa kusema kuwa ni muhimu pia kuzingatia mlo kamili wakati wa kuandaa chakula cha watoto pindi wanapotimiza umri wa miezi 6 na kuendelea ili kuepuka changamoto ya utapiamlo hususani tatizo la udumavu wa mwili na akili kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

