Naibu Waziri Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb) kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) atoa wito kwa watanzania kutumia fursa ya kujifunza utaalamu na teknolojia za kisasa kutoka kwa makampuni ya mbalimbali.
Mhe. Kigahe Ameyasema hayo tarehe 23 Februari, 2023 aliposhiriki hafla ya ufunguzi wa maonesho ya 24 ya sekta ya ujenzi, madini na miundombinu ya Build Expo Africa katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam.
Mhe. Kigahe amesema kuwa maonesho hayo ya siku tatu yaliyoanza tarehe 23 Februari, 2023 yanalenga kuleta mapinduzi ya kiuchumi katika eneo la ujenzi, uchimbaji madini, gesi na mafuta katika eneo la Afrika Mashariki hivyo hii ni fursa ya watanzania kushirikiana na wawekezaji kutoka nchi mbalimbali ambao wamekuja kuonesha teknolojia zao kupata ujuzi wa kuanzisha Kampuni hizo.
Naye Waziri wa Mafuta na Maliasiri wa Somalia Mhe. Abdirizak Omary Mohamed amesema kuwa mazingira ya uwekezaji kwa Tanzania yameboreswa sana na kila mwekezaji anatamani kuwekeza hapa hivyo anawaalika pia wawekezaji wa kitanzania kuwekeza nchini Somalia kwani kuna fursa nyingi.
Mhe. Mohamed ameongeza kuwa kupitia maonesho haya makampuni ya Somalia yamepata fursa ya kuonesha shughuli mbalimbali zinazofanywa za uwekezaji hasa katika eneo la Mafuta na gesi.
Ufunguzi wa Maonesho hayo ya Build Expo Africa yamehusisha Makampuni zaidi ya 150 na nchi zaidi ya 35 ambapo pia yamehudhuriwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Somalia Mhe. Mohamed Hussein Roble, Waheshimiwa mabalozi, Taasisi ya Sekta binafsi Tanzania (TPSF), Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA).