TANZANIA YAUNGA MKONO AZIMIO LA UIMARISHAJI WA HUDUMA ZA CHANJO KWA WATOTO.

MUUNGANO   MEDIA
0

Na WAF- Addis Ababa, Ethiopia

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (Mb), ameshiriki kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Mkutano wa pembeni kuhusu Uimarishaji wa utoaji wa huduma za chanjo kwa Watoto katika nchi za Afrika baada ya mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19. 

Mkutano huo uliowahusisha Wakuu wa nchi wa umoja wa Afrika wenye lengo la kuimarisha utoaji wa chanjo kwa watoto, umeendelea katika Jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Katika Mkutano huo imeelezwa kuwa, kufuatia janga la COVID-19 kumekuwa na ongezeko la watoto ambao hawakupatiwa chanjo kutoka watoto milioni 7.7 mwaka 2020 hadi watoto miloni 12 mwaka 2022, Hali iliyosababisha kuongezeka kwa milipuko ya magonjwa yanayoweza kuzuilika kwa chanjo ikiwemo Surua na Polio, hii ni kwa mujibu wa WHO-AFRO).

Kikao hiki kimezitaka Nchi zote za Afrika kuimarisha utoaji wa chanjo kwa watoto wote ili kuhakisha magonjwa yote yanayoweza kuzuilika kwa chanjo yanamalizika ikiwemo Surua na POLIO. 

Sambamba na hayo, kikao hicho kimetaka agenda ya Chanjo kwa watoto ibebwe na kila nchi husika na kuwa tayari kuongeza rasilimali fedha za ndani kwa ajili ya huduma za chanjo. 

Kwa upande wake Waziri wa Afya nchini Tanzania, Mhe. Ummy ameeleza, Serikali ya Tanzania itaendelea kushirikiana na wadau wote wakiwemo Sekta binafsi, Hospitali za binafsi, Taasisi za dini, Mashirika yasiyo ya kiserikali kutoa huduma za chanjo ili kuwafikia watoto wengi na hatimaye kumaliza kabisa magonjwa yote yanayoweza kuzuiliwa kwa kutumia chanjo. 

Aidha, Waziri Ummy ameeleza kuwa Tanzania itatumia njia mbalimbali ikiwemo nyumba kwa nyumba ili kuwafikia watoto wote ambao hawajapata chanjo ili kuwakinga dhidi ya magonjwa mbalimbali yanayoweza zuilika kwa afua hiyo ya chanjo.

Mashirika ya kimataifa yanayohusika na utoaji wa Chanjo ikiwemo UNICEF, GAVI na WHO yameahidi kuendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa nchi zote za Afrika ili kuhakikisha watoto wengi wanafikiwa kwa kupata chanjo. 

Aidha, mashirika yanayosimamia upatikanaji wa chanjo, yahakikishe wanasimamia wazalishaji ili kuondoa tatizo la kutopatikana kwa chanjo kwenye maeneo yote.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)