Na WyEST, BUTIAMA - MARA.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) kilichopo Butiama kitaanza kudahili wanafunzi mwaka huu 2023 katika fani za kilimo na teknolojia.
Ameyasema hayo Wilayani Butiama mkoani Mara wakati alipotembelea kukagua maendeleo ya chuo hicho na kukitaka chuo hicho kujikita kwenye kutoa mafunzo ya kilimo kwa upana wake ambao ndio msingi halisi wa uanzishwaji chuo hicho.
Waziri Mkenda pia ameelekeza chuo hicho kufanya tafiti kwenye eneo la kilimo na kusambaza matokeo ya tafiti hizo ili yaweze kunufaisha wakulima mahali walipo kwa kuongeza tija na uzalishaji.
Mkenda ameongeza kuwa mikakati mbalimbali itatumika kuhakikisha wanafikia vigezo vya kupata ithibati ili kuruhusu kutoa mafunzo ikiwemo kuongeza wanataaluma na kuweka mazingira na miundombinu stahiki ya kufundishia na kujifunzia.
"Tutahakikisha MJNUAT Butiama kinaanza kutoa Mafunzo mwaka huu 2023, tayari Serikali imetoa Shilingi bilioni 2.6 kwa ajili ya kukarabati majengo yaliyopo na kujenga hosteli mpya 2 ili wanafunzi watakapoingia wakae katika mazingira bora," amefafanua Waziri Mkenda.
Profesa Mkenda ameongeza kuwa Serikali pia imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 102 kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kwa ajili ya kujenga makao makuu ya Chuo hicho hapo hapo Butiama.


