Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa sasa imefanikiwa kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa wa kifua kikuu nchini kwa asilimia 55 ukilinganisha na asilimia 75 ya malengo ya kupunguza vifo hivyo ifikapo mwaka 2025.
Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dodoma na Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu na Ukoma kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Peter Neema katika uzinduzi wa Mapitio ya Muhula wa Kati wa Mpango Mkakati wa Taifa nchini awamu ya sita.
Dkt. Peter amesema wanafanya Mkakati wa kuongeza mashine za maabara na kutoa elimu kwa ajili ya kupima vina saba vya kifua kikuu ili kufikia lengo la uibuaji wa ugonjwa huo.
Aidha ameeleza kuwa wanatarajia kufanyia maboresho katika Mpango Mkakati wa Sita ili kuchukuaa hatua zilitolewa katika ripoti na kuwezesha kufikia malengo ifikapo mwaka 2025.
''Sasa hivi tunategemea kufanyia maboreshi katika mpango mkakati wetu wa sita ili kuchukua mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti na tuweze kufikia malengo yetu vizuri tutakapofika mwisho wa mpango mkakati huu 2025'' amesema Dkt. Peter.
Katika hatua nyingine Dkt.Peter amesema kumekuwa na changamoto kwenye uibuaji wa maambukizi mapya ya kifua kikuu, kutokana wagonjwa wengi kukosa elimu bora juu ya uibuaji wagonjwa hao.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Shidefa Plus Kutoka Mkoani Shinyanga, Bi. Radia Khaji amesema wanatumia wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii kwenda kutoa elimu juu ya Kifua Kikuu pamoja na kufanya uchunguzi wa awali kwa wachimbaji wa madini wenye dalili za gonjwa huo ili kusababisha kufanyiwa uchunguzi zaidi katika vituo vya kutolea huduma za afya .


