Na Emmanuel Kawau.
Wizara ya Nishati imekabidhi kibali cha ujenzi wa Bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki kwa kampuni ya EACOP Tanzania LTD kwa niaba ya serikali kwaajili ya kuanza Ujenzi wa Bomba la mafuta ghafi kutoka Mtukula Nchini Uganda hadi Chongoreani,Tanga, Tanzania.
Akizungumza Katika hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika Jijini Dar es Salaam Waziri Wa Nishati Januari Makamba amesema mchakato wa kukabidhi kibali hicho umezingatia masuala ya utunzaji wa mazingira pamoja na utafiti uliofanyika kwa kina .
Hata hivyo amesema Mikoa yote minane ambayo bomba hilo litapita wote watanufaika,kwani tayari mradi umeanza kutekelezwa kwa kulipa fidia kwa wakati, kaya zaidi ya 9800 wameshalipwa fidia.
“Tayari tumelipa fidia shilingi bilioni 29, na mradi huu umeanza kutekelezwa katika baadhi ya maeneo, mfano kununua vifaa, kuanza ujenzi wa vituo vya kuhifadhia mafuta Mkoani Tanga. kwa hiyo tunatarajia mradi huu ulete ajira nyingi za moja kwa moja lakini pia ajira za kutoa huduma kama vile hoteli, hivyo Watanzania wachangamkie fursa hiyi” amesema Waziri Makamba.
Aidha ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA) ambayo imepewa asilimia 15% ya usimamizi wa mradi huo kwenye kampuni ya EACOP kuhakikisha inatangaza fursa zilizopo pamoja na kusimamia ipasavyo sheria ya Local Content kwa kuhakikisha wazawa wanapata fursa mbalimbali zitokanazo na mradi huo na kuhakikisha wazawa wanafaidika na mradi.
Awali akizungumza Katika hafla hiyo Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Nishati na Maji EWURA Dkt James Andilile amesema Mamlaka hiyo imepewa jukumu ambalo watahajikisha wanatekekekele vizuri maagizo waliyopewa na kuhakikisha wanasimamia vema mradi na kuisha kwa wakati.
"Kampuni ya EACOP imepewa zabuni hiyo kutokana na kukidhi masharti ya kimkataba ikiwemo kuzingatia masuala ya utunzaji wa mazingira, Athari za kibinadamu, pamoja na uwezo wa kitaalamu na kifedha kwa ajili ya kutekeleza mradi"amesema Mkurugenzi
“Ujenzi huu wa kipande cha kutoka Mtukula hadi Chongoreani Mkoani Tanga una urefu wa kilomita 1147 , sisi kama EWURA tuna matumaini kwamba kampuni ya EACOP TZ itaendelea kuzingatia yote tuliyokubaliana kabla na baada ya ujenzi wa Bomba hili” amesema Dkt Andilile.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omary Mgumba akizungumza kwa niaba ya wakuu wa mikoa nane ambayo mradi huo utapita ambayo ni Tanga, Manyara, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Geita na Kagera,amesema watahakikisha wanasimamia vema miundombinu ya mradi huo kwa kutumia Jeshi la Akiba katika ulinzi hivyo wameomba Serikali kujenga vituo vya polisi katika vituo vya kuhifadhia mafuta ghafi ili kuhakikisha ulinzi na usalama unakuwepo wakati wote wa Ujenzi na baada ya kukamilika.
Nae Naibu Mkurugenzi wa Kampuni ya EACOP Tanzania ambayo imekabidhiwa Kibali cha ujenzi wa mradi huo Bi. Wendy Brown amesema kuwa Kampuni hiyo iko vizuri katika Ujenzi wa Miundombinu ya kuunganisha Nchi Kwa nchi kibiashara na hiyo watahakikisha wanazingatia makubaliano ya mkataba hadi Mradi kukamilika.

