Na Gideon Gregory, Dodoma.
Katibu Mtendaji Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Prof. Charles Kihampa amesema kuwa tume hiyo imefanikiwa kuongeza idadi ya Wanafunzi wanaosoma katika vyuo vya elimu ya juu kutoka 259,266 mwaka 2020/21 hadi 295,919 mwaka 2021/22 sawa na asilimia 14.1 huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka kwa mwaka wa masomo 2022/2023.
Prof. Kihampa amebainisha hayo leo Februari 22,2023, Jijini Dodoma katika kikao na waandishi wa habari Wakati akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Tume hiyo katika kipindi cha serikali ya awamu ya Sita chini ya Mh. Dkt Samia Suluhu Hassan.
Amesema Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa kama yalivyoainishwa katika Sheria ya Vyuo Vikuu, Sura ya 346 ya Sheria za Tanzania.
“Mafanikio haya ni kielelezo na uthibitisho wa jinsi serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ilivyoiwezesha TCU kuweza kutekeleza vizuri majukumu yake kwa mujibu wa sheria, kanuni, miongozo na taratibu za uendeshaji wa vyuo vikuu hapa nchini, kikanda na kimataifa,”amesema.
Aidha, ameongeza kuwa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania imeimarisha mifumo yake ya kielektroniki inayotumika katika utoaji wa huduma mbalimbali kwa wadau mbalimbali wa elimu, ambapo baadhi ya mifumo hiyo ni pamoja na mfumo wa pamoja wa kielekroniki kwa ajili ya kuratibu udahili wa shahada za kwanza kwa vyuo vyote vya elimu ya juu hapa nchini, mfumo wa Utambuzi wa Tuzo za Wahitimu kutoka Vyuo Vikuu vya nje ya Tanzania na mfumo wa kuchakata maombi ya Hati ya Kutokuwa na Pingamizi kwa wananchi wanaotaka kwenda kusoma vyuo vikuu nje ya nchi.
Amesema maboresho hayo ya mifumo yameongeza tija na ufanisi na kurahisisha utoaji wa huduma kwa kuwawezesha wananchi na wadau mbalimbali kupata huduma bora na kwa haraka.
“Kwa mfano, muda wa uhakiki na utambuzi wa tuzo za nje ya nchi umepungua kutoka siku 14 za awali hadi siku tatu, pia waombaji wa udahili wanaweza kutuma maombi yao moja kwa moja kwenye vyuo husika na kuthibitisha vyuo wanavyopenda popote walipo bila kulazimika kusafiri kwenda chuoni,”amesema.
Pia amesema katika kuhakiki ubora, TCU imeimarisha mifumo yake ya ushauri na ukaguzi wa mara kwa mara, wa kawaida na wa kushtukiza kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo kwa lengo la kuhakikisha kuwa elimu itolewayo na vyuo vikuu hapa nchini inakidhi viwango vya ubora kitaifa, kikanda, na kimataifa. Kwa mfano, katika kipindi cha Julai 2021 hadi Februari, 2023 vyuo vikuu vyote 47 vilivyopo vimekaguliwa na kupewa ushauri wa maeneo yanayohitaji kuboreshwa.
“Zoezi hili la ukaguzi wa vyuo ni endelevu kila mwaka. Vilevile TCU imeweka utaratibu wa kuanzishwa na kuimarishwa mifumo ya uthibiti ubora ndani ya vyuo vikuu ambapo vyuo vyenyewe vimekua na utaratibu wa kujikagua, kujitathmini na kufanya marekebisho mbalimbali kwa kuzingatia miongozo ya uendeshaji wa vyuo vikuu,”amesema.
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ni Taasisi ya Serikali, iliyoundwa mwaka 2005 kwa Sheria ya Vyuo Vikuu, Sura ya 346 ya Sheria za Tanzania ambapo ilitokana na maboresho yaliyofanywa na Serikali kwa lililokuwa Baraza la Ithibati la Elimu ya Juu (HEAC) lililoanzishwa mwaka 1995 kwa Sheria ya Elimu Sura ya 523 ya Sheria za Tanzania.


