FURSA ZA MAFUNZO KWA WATANZANIA NJE YA NCHI NI MATOKEO YA MAHUSIANO MAZURI YA KIDIPLOMASIA YANAYOJENGWA NA RAIS MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN

MUUNGANO   MEDIA
0

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema fursa za mafunzo kwa Watanzania zinazopatikana nje ya nchi zikiwemo za watumishi wa umma ni matokeo ya mahusiano mazuri ya kidiplomasia na wadau wa maendeleo yanayojengwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Jenista amesema hayo jijini Dodoma, wakati akizungumza na watumishi wa umma walionufaika wa mafunzo nchini Korea yanayofadhiliwa na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Serikali ya Korea (KOICA).

Mhe. Jenista amesema, kumekuwa na ongezeko la fursa za mafunzo ya muda mrefu na mfupi nchini Korea, China na India ambazo ni matunda ya kazi nzuri ya kuboresha mahusiano ya kidiplomasia na wadau mbalimbali wa maendeleo yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita.

Akizungumzia umuhimu wa fursa hizo za mafunzo, Mhe. Jenista amesema Serikali itazitumia ipasavyo kuendeleza rasilimaliwatu iliyopo ile iendane na kasi ya maendeleo ya teknolojia, ambayo hivi sasa ina nafasi kubwa ya kuongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa watumishi wa umma. 

“Watakaonufaika na fursa hizi za mafunzo, ndio watakaolisaidia taifa kuendana na kasi ya maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na hata ukiwasikiliza vizuri wanufaika hawa utabaini kuna maarifa ya ziada waliyoyapata ambayo yatawasaidia kuongeza ufanisi kiutendaji,” Mhe. Jenista amesisitiza. 

Mhe. Jenista amefafanua kuwa, nchi ya Korea ina utamaduni mzuri wa ufanyaji kazi katika Utumishi wa Umma, hivyo waliobahatika kupata mafunzo nchini humo watakuwa ni chachu ya kuboresha utendaji kazi nchini na kuondokana na ufanyaji kazi wa mazoea wa baadhi ya watumishi wa umma, na kuongeza kuwa fursa za mafunzo zikiongezeka na wanufaika wakitumika vizuri ni dhahiri kuwa taifa litapiga hatua kimaendeleo.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)