Na.Faustine Gimu Galafoni,Chemba Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amewataka watumishi wa halmashauri ya Chemba kujitafakari katika utumishi wao kutokana na halmashuri hiyo kurudi nyuma kimaendeleo kwa kudorora ukusanyaji wa mapato,kiwango cha chini ufaulu na miradi mbalimbali kutotekelezwa kwa wakati, chanzo kikitajwa kuwa ni malumbano na mivutano isiyo na tija kwa watumishi wa halmashauri hiyo.
Mkuu wa Mkoa huyo amebainisha hayo Wilayani Chemba Mkoani Dodoma baada ya kufanya mkutano na Watumishi wa halmashauri hiyo ngazi ya vijiji hadi wilaya lengo ni kusikiliza kero pamoja na changamoto mbalimbali zinazosababisha halmashuri hiyo kusuasua katika nyanja mbalimbali zikiwemo nyanja za elimu,Kilimo ,na miradi mbalimbali ya maendeleo kukwama kutokana na malumbano kwa viongozi wanavyoeleza.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Said Sambala ,diwani wa kata Jangalo Abdu Msuri ,diwani wa kata ya mrijo Abdallah Satti pamoja na mjumbe kamati ya fedha Mwanahamis Batu wamesema malumbano ya kila siku imekuwa changamoto katika halmashauri hiyo.
Mbunge wa jimbo la Chemba Mohammed Moni naye amekiri kuwa baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo wamekuwa vikwazo kwani wamekuwa wakipuuza hata ushauri unaotolewa .
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka amemtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuwa makini na ushauri wa upotoshaji anaopewa na baadhi ya watumishi wake hususan wakuu wa idara.
Hivyo,Mkuu huyo wa mkoa amewataka watumishi wa halmashauri ya Chemba kujitafakari kwani halmashauri haiwezi kuendeshwa kwa malumbano.
Katika kuhakikisha Wilaya ya Chemba inasonga mbele kimaendeleo ,amewataka viongozi kuibua miradi kwa kuangalia mashamba kwa vijiji na shule zenye wazalishaji wakubwa wa mazao ili aweze kufanya ziara na kuweka mikakati imara ya namna ya kuvisaidia vijiji na maeneo hayo kukuza uzalishaji.
Kuhusu suala la watendaji wa vijiji na kata kubambikiziwa madeni kutokana na hitilafu ya mifumo ya mashine ya kukusanyia mapato kuwa na changamoto ya kujirudiarudia utoaji wa stakabadhi mkuu huyo wa mkoa ameagiza wafutiwe madeni mara moja kwani hiyo ni kuwakatisha tamaa huku akikitaka kitengo cha TEHAMA kufanya uhakiki wa mashine hizo na kubaini kasoro zilizojitokeza.
Kuhusu suala la Elimu wilayani Chemba ,Mkuu huyo wa mkoa amesema haiwezekani shule iwe na wanafunzi 13 halafu baadhi yao wafeli mtihani hivyo ni vyema wadau wa elimu Chemba kuja na ubunifu katika kuhakikisha kiwango cha elimu kinaongezeka .
MWISHO.
Chapa KAZI RC mtaka tunakuaminia
JibuFuta