
- Aagiza
masoko zaidi ya wamachinga yajengwe
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ana dhamira ya dhati kuhakikisha kila Mtanzania
anapata fursa sawa ya kufanya biashara katika mazingira bora na rafiki kwa
biashara ili kukuza uchumi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo (Jumatano, Machi 9, 2022) wakati
alipotembelea mradi wa ujenzi wa Soko la Wafanyabiashara Wadogo (Machinga
Complex) lililoko barabara ya Bahi Mkoani Dodoma na kusema ameridhishwa na
ujenzi wa soko hilo.
"Lengo la maboresho haya kwa wafanyabiashara wadogo ni
kutaka kutengeneza fursa zaidi kwa kuwa na maeneo salama yanayotambulika
na yanayoweza kutumika na taasisi za kifedha kutoa mikopo na fursa nyingine za
kiuchumi."
Waziri Mkuu ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Dodoma kwa ubunifu na
kuwataka viongozi hao waendelee kusimamia mradi huo na kuukamilisha kwa wakati
pamoja na kubuni maeneo mengine ya nje ya mji Ili kukuza maeneo mengi zaidi
kibiashara katika mkoa huo.
AIdha, Waziri Mkuu amewataka wafanyabiashara wadogo wa mkoa huo
wafuate utaratibu utakaowekwa na mkoa huo mara baada ya ujenzi kukamilika.
"Serikali imeendelea kutafuta fursa za kifedha kwa wafanyabiashara wadogo,
hivyo jipangeni kutumia fursa hizo kwa uaminifu."
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-
(TAMISEMI), Innocent Bashungwa amesema Mkoa wa Dodoma umefanya kazi kubwa ya
kutekeleza mradi rafiki kwa wamachinga wa mkoa huo. “Niwasihi wakuu wa mikoa
mingine kuiga mfano huu kwa kujenga miradi ya kuwapanga machinga kulingana na
mazingira yaliyo katika mikoa yenu.”
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa
vijana kuendelea kutumia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali ili waweze
kujikwamua kiuchumi.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amesema mradi huo
utakapokamilika mwezi mei, machinga wote walioko katika maeneo ya jiji la
Dodoma watahamishiwa kwenye eneo hilo rasmi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Bw. Joseph
Mafuru amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika Mei mwaka huu na utagharimu
shilingi bilioni 7.5 hadi kukamilika kwa awamu zote huku akisema kuwa mradi huo
utakuwa na manufaa makubwa kwani utaiwezesha Halmashauri kukusanya shilingi
bilioni 1.1 kwa mwaka.
Nao, wafanyabiashara ndogondogo ambao ndio wanufaika wa mradi
huo wameishukuru Serikali kwa kuwezesha ujenzi wa mradi huo na kwamba wako
tayari kupokea maelekezo ya mkoa na kufanya biashara katika eneo hilo.