CHANGAMTO YA BARABARA USHETU

0

Naibu waziri wa ujenzi Elias Kwandikwa  amewahakikishia wananchi wa kata ya Ulewe  halmashauri ya Ushetu  mkoani Shinyanga kuimarisha miundombinu ya barabara ambayo imekuwa changamoto katika kata hiyo ikiwa ni pamoja na ukarabati wa Daraja la Ilangashika.

Akizungumza na wananchi  wa kata  Ulewe  katika eneo ya daraja hilo ambalo limekuwa kikwazo kikubwa cha  maendeleo Kwandikwa amesema kuwa baada ya kukamilisha maeneo yaliyo kuwa na changamoto kubwa yakiwemo madaraja ya Kalo,Kasheshe na Kidanha  ambayo yamegharimu pesa nyingi sasa ni wakati wa kushughulikia miundombinu ya Ilangashika.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Ulewe Kulwa Emmanuel  ameiambia Baloha FM kuwa ujio wa Naibu waziri huyo  wa ujenzi ni faraja kwa wananchi ambapo amebainisha kuwa daraja hilo linamekuwa adha kubwa kwani limekuwa likisababisha magari mengi kuharibika na nauli kuwa ghali.

Katika hatua nyingine Naibu waziri wa Ujenzi Elias Kwandikwa  amesema kuwa kukamilika kwa barabara ya mkato ya  Mseki Bulungwa itarahisisha kufika makao makuu ya Halmashauri ya Ushetu kwa haraka zaidi  hivyo itafungua wigo wa uchumi  endapo itapanuliwa na kukarabatiwa.


Kwandikwa tangu  ateuliwe  kuwa  Naibu waziri  wa ujenzi  Mwaka huu ,ameshabakiza kufanya ziara mikoa 7 pekee ili  kuieneza Tanzania nzima ambapo leo anaendelea na ziara katika halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga kwa lengo la kujionea miundombinu ya barabara na kufanya tathmini ya gharama za ujenzi akiwa na watalaam  kutoka Mamlaka ya barabara mjini na vijijini TARURA na TANROADS.

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)