IKIFIKA OKTOBA TWENDENI TUKAPIGE KURA – JENESTA MALINGO

MUUNGANO   MEDIA
0

 


Na Mwandishi Wetu- Dodoma.


Mgombea wa udiwani kata ya Zuzu (Nzinje), Bi Jenesta Project Malingo, amechukua rasmi fomu ya kugombea nafasi hiyo leo Agosti 19, 2025 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuahidi kuwaletea wananchi maendeleo yenye kasi, mshikamano na ushirikishwaji.


Bi Jenesta ambaye awali alikuwa Katibu wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT) kata ya Zuzu, alisema wanachama wote wameunganishwa kwa lengo moja la ushindi wa CCM.


“Mchakato ulikuwa na hekaheka, mambo yalikuwa mengi, lakini tumefika leo na tunatangaza kuwa hakuna makundi tena. Wote ni kitu kimoja. Naomba wananchi wa kata ya Zuzu tushirikiane, ikifika Oktoba tupige kura kwa Mhe. Rais Samia, Mbunge atakayeteuliwa na kwa upande wa kata yetu – Jenesta Project Malingo,”alisema kwa kujiamini.


Mwenyekiti wa CCM kata ya Zuzu, Omari Bilali Kagusa, alisisitiza kuwa uchaguzi ndani ya chama ni jambo la kawaida na makundi lazima yafutwe mara tu mgombea rasmi anapopatikana.


“Tusidanganyane, kila mmoja alikuwa na wa kwake, lakini sasa wa kwetu ni Jenesta Project Malingo. Kumpinga ni sawa na kukisaliti chama. Tushirikiane, tuweke CCM madarakani,” alisema Kagusa kwa msisitizo huku akishangiliwa na wanachama.


Naye Mwenyekiti wa UWT kata ya Ipagala, Amina Hassan Mpole, alisema wanawake na wanachama wote wa CCM wanapaswa kusimama imara kuhakikisha ushindi wa mgombea huyo.


“Leo Jenesta ameweka historia kwa kuchukua fomu. Tumeunganishwa na mgombea mmoja pekee. Tukifanya uzembe tutakiangusha chama, siyo yeye. Ushindi wake ni ushindi wa CCM,” alisema.


Katibu wa CCM kata ya Zuzu, Suma Kyomola, aliwataka wanachama wote kutumia nguvu zao kuhakikisha chama kinashinda kwa kishindo.


“Katika mchakato walikuwepo wagombea zaidi ya 20, lakini ilibidi mmoja apatikane. Sasa nguvu zetu zote zielekezwe kwa Jenesta. Msikubali kurubuniwa na vyama pinzani, kumbukeni nguvu ya ushindi wa CCM unatokana na wanachama wake,” alisema.


Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Siasa, Elias Nkwabi, aliwaonya wanachama kutokuwa na misuguano au kuruhusu makosa ambayo yanaweza kudhoofisha chama.


“Ushindi wa CCM ni kama mboni ya jicho. Tukikosea tukaruhusu kata iende kwa wapinzani, tutakuwa tumedhihirisha udhaifu mkubwa. Tunatakiwa kushirikiana, kumheshimu mama yetu Samia, mbunge wetu na diwani kutoka CCM – hiyo ndiyo mnyororo wa mafiga matatu unaolinda chama chetu,” alieleza.


Akihitimisha, Bi Jenesta Malingo aliwataka wanachama wote na wananchi wa kata ya Zuzu kujitokeza kwa wingi katika kampeni na uchaguzi ili kuhakikisha chama kinabaki na historia yake ya kushinda udiwani katika kata hiyo.


“Zuzu imekuwa ngome ya CCM kwa muda wote. Naahidi kuwa diwani wa mshikamano, ushirikishwaji na maendeleo ya kweli kwa wananchi wa Nzinje. Umoja wetu ndiyo ushindi wetu,” alisema kwa hamasa.


Kwa miaka yote tangu kuanzishwa kwa serikali za mitaa, kata ya Zuzu haijawahi kuongozwa na chama kingine zaidi ya CCM, jambo linalotoa ishara ya kuendeleza historia hiyo kupitia mgombea mpya – Jenesta Project Malingo.

Kauli mbiu ya Jenesta: “Maendeleo yenye kasi, mshikamano na ushirikishwaji wa wananchi.”














Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)