Jeshi la Polisi limesema limepokea agizo la Waziri wa Maliasili na
Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla la kuwachukulia hatua watu wanne ndani ya siku
saba kwa madai wanashiriki katika mtandao wa ujangili, lakini halifanyi kazi
kwa shinikizo.
Msemaji wa Jeshi hilo, Barnabas
Mwakalukwa amesema polisi wanafanya kazi kwa kufuata kanuni, taratibu na
sheria za Jeshi hilo.
Juzi, Kigwangalla
mbali na kutoa agizo hilo, amesema watu hao wanne pia walipanga njama za kumuua
mwanaharakati, Wayne Lotter na kwamba polisi wakishindwa kuwakamata atawashtaki
kwa Amiri Jeshi Mkuu ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwakalukwa amesema jukumu lao ni kukamata wanapopata
shitaka la kuwapo kwa kitu kisicho cha kawaida, kuchunguza na kupeleka kwa
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya kukamilisha taratibu nyingine.