Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) linawakaribisha wananchi wanaotembelea Maonesho ya Nane Nane Jijini Dodoma kutembelea banda lake ili kujionea huduma mbalimbali za mawasiliano na teknolojia ya kidijitali, hususan huduma ya Faiba Mlangoni (FTTH) inayowezesha upatikanaji wa intaneti ya kasi kubwa majumbani, ofisini na kwenye biashara.
TTCL inaendelea kusogeza huduma zake karibu na wananchi kwa lengo la kuunga mkono maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.
Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa Biashara TTCL Dodoma Bi. Leyla pongwe amesema huduma ya Faiba Mlangoni imeboreshwa ili kuwapatia wananchi intaneti ya uhakika kwa matumizi ya masomo mtandaoni, mikutano ya video, biashara za kidijitali, burudani na huduma nyingine zinazohitaji kasi kubwa ya intaneti.
Aidha,Bi.Lyela amewasihi wananchi kutembelea banda la TTCL ili kupata elimu kuhusu namna ya kujiunga na huduma ya Faiba Mlangoni, kujisajili papo hapo pamoja na kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa shirika kuhusu suluhisho mbalimbali za mawasiliano na TEHAMA.
"TTCL inawahimiza wakulima kutumia fursa ya Maonesho ya Nane Nane kutembelea banda lake na kujionea teknolojia za kisasa zitakazorahisisha shughuli za kila siku na kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa mazao, biashara na utoaji wa huduma."amesema.



