e-GA YASAJILI ZAIDI YA VYAMA 6,000 KIDIJITALI.

MUUNGANO   MEDIA
0

 



Na Avelina Musa - Dodoma.


Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) imesema matumizi ya mifumo ya kidijitali katika vyama vya ushirika yameleta mapinduzi makubwa katika usimamizi wa shughuli za ushirika nchini, huku zaidi ya vyama 6,000 vikisajiliwa kwenye mfumo maalum wa kidijitali.


Hayo yamesemwa leo August 2 ,2026 na Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Serikali Mtandao(e-GA) Bi.Subira Kaswaga,wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma.


 Amesema kuwa mfumo huo umewezesha kuongeza uwazi katika biashara za mazao, kupunguza mianya ya upotevu wa mapato pamoja na kuwapa wakulima uwezo wa kufuatilia mwenendo wa mauzo ya mazao yao kwa wakati na umetengenezwa kwa ushirikiano na Tume ya Maendeleo ya Vyama vya Ushirika kwa lengo la kurahisisha uendeshaji wa shughuli za ushirika kupitia teknolojia.


"Kupitia mfumo huu mkulima anaweza kupata taarifa kuhusu mazao aliyowasilisha, bei iliyopatikana sokoni pamoja na kiasi cha fedha anachopaswa kulipwa, jambo ambalo limeongeza uwajibikaji na kuimarisha uaminifu kati ya wakulima na vyama vya ushirika."amesema.


Amesema mfumo huo umeongeza uwezo wa serikali kufuatilia mwenendo wa soko la mbolea na kusaidia kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo hizo kwa bei inayozingatia maelekezo yaliyowekwa.


Kaswaga amesema mamlaka hiyo imeshirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuanzisha mfumo wa Fertilizer Information System (FIS), ambao unasaidia serikali kufuatilia mnyororo wa upatikanaji wa mbolea kuanzia wazalishaji, waagizaji hadi wasambazaji.


Aidha, ameongeza kuwa e-GA imeendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na taasisi mbalimbali kuandaa na kuboresha mifumo ya kidijitali inayosaidia ukusanyaji wa taarifa za wakulima, utoaji wa huduma na usimamizi wa shughuli mbalimbali za kilimo.


Mwisho.

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)