Na Avelina Musa - Dodoma.
Bodi ya Bima ya Amana (DIB) imesema amana za wateja katika benki na taasisi za fedha zilizopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinalindwa kwa kiwango cha hadi shilingi milioni 7.5 endapo benki itafilisika au kufutiwa leseni.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa DIB, Lwaga Mwambande, amesema kiwango hicho kinahakikisha mteja mwenye amana zisizozidi shilingi milioni 7.5 analipwa fedha zake zote ikiwa benki yake itafungwa.
Amesema mfuko wa bima ya amana huchangiwa na benki na taasisi za fedha zinazopokea amana kutoka kwa wananchi, ambapo kila benki huchangia asilimia 0.15 ya jumla ya amana zake mara moja kwa mwaka.
Mwambande amesema fedha zinazokusanywa huwekezwa katika dhamana za Serikali na maeneo mengine ya uwekezaji ili kuhakikisha mfuko unakuwa na uwezo wa kulipa fidia kwa wateja pale benki inaposhindwa kuendelea na shughuli zake.
Amesema kwa sasa Bodi inaendesha ufilisi wa benki tisa zilizofungwa kati ya mwaka 2000 na 2018 ambazo ni Greenland Bank, Delphis Bank, FBME Bank, Efatha Bank, Covenant Bank for Women, Mbinga Community Bank, Njombe Community Bank, Meru Community Bank na Kagera Farmers Cooperative Bank.
Kwa upande wake, Meneja wa Fedha na Uhasibu wa DIB, Romuli Mtui, amesema ufilisi wa benki saba zilizofungwa mwaka 2017 na 2018 bado unaendelea katika hatua mbalimbali.

