DIB YAWAITA WATANZANIA KATIKA MAONESHO YA NANE NANE ILI KUPATA ELIMU KUHUSU MFUMO WA KULINDA FEDHA.

MUUNGANO   MEDIA
0

 


Na Avelina Musa - Dodoma.

BODI Ya Bima Ya Amana Tanzania (DIB) imewataka wananchi kutembelea banda  Hilo katika maonesho ya nane nane Jijini Dodoma ili kupata elimu kuhusu mfumo wa Bima ya Amana unaolenga kulinda fedha za wawekaji wa amana katika taasisi za fedha zilizo chini ya mfumo huo.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mkuu wa DIB,Isack Kihwili wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea banda hilo lililoko katika maonesho ya Nanenane Jijini Dodoma.



 Amesema wananchi wanaoweka fedha katika taasisi zisizo na leseni ya BoT wanajiweka katika hatari ya kutokuwa na uhakika wa kupata fidia endapo taasisi hizo zitashindwa kuendelea na shughuli zake.


 Kihwili amewataka wawekaji wa amana wa FBME ambao bado wana madai kufika katika banda la DIB kuwasilisha madai yao, ambapo watapatiwa fomu maalumu za kujaza kwa ajili ya kuanza mchakato wa kushughulikiwa kwa madai yao.


Amewataka wananchi kuwa makini katika kuchagua taasisi za fedha wanazoweka fedha zao, akisisitiza umuhimu wa kutumia benki na taasisi zilizopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kulinda haki zao za kupata fidia endapo taasisi hizo zitakumbwa na changamoto za kifedha kuhusu mchakato wa ufilisi wa benki.

Amesema utaratibu huo umeonyesha umuhimu wake kupitia wateja wa Benki ya FBME ambao walinufaika na mfumo wa fidia uliowekwa na Serikali.


Kihwili amesema sheria imeweka utaratibu maalumu wa namna madai yanavyolipwa, ambapo gharama za ufilisi, kodi pale zinapohusika na stahiki za wafanyakazi huzingatiwa kabla ya kushughulikia makundi mengine ya wadai.

“Wenye amana ni miongoni mwa wanaoshughulikiwa katika utaratibu huo, huku kukiwa na makundi mengine ya wadai, wakiwemo waliokuwa wamefungua kesi dhidi ya benki hiyo na kushinda, pamoja na wazabuni,” amesema.

Kihwili amesema wateja wa FBME ambao si wenye amana, wakiwemo wadai waliokwenda mahakamani kudai fedha zao, hawatalipwa katika awamu ya sasa inayolenga kuwalipa wenye amana.





Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)