Wizara ya Afya, kupitia Idara ya Kinga, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma (Health Promotion Section - HPS), imepokea vifaa vya mfumo wa matangazo ya sauti (Public Address System-PA) vyenye thamani ya takribani Shilingi za Kitanzania milioni 145.8 (Dola za Kimarekani 54,000), vilivyotolewa na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) kupitia Pandemic Fund.
Vifaa hivyo vinatarajiwa kuboresha utoaji wa elimu ya afya kwa umma pamoja na kuimarisha mawasiliano wakati wa majanga ya afya na milipuko ya magonjwa nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea vifaa hivyo , Julai 8, 2026 mkoani Dodoma Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Eliud Eliakim amesema msaada huo unaonesha dhamira ya pamoja ya Serikali na wadau wa maendeleo katika kuendelea kuimarisha uwezo wa nchi kwenye mawasiliano ya hatari na ushirikishwaji wa jamii (Risk Communication and Community Engagement – RCCE).
Amesema lengo ni kujenga jamii yenye uelewa mpana, inayopata taarifa sahihi na yenye utayari wa kukabiliana na changamoto mbalimbali za afya ya umma.
"Tunapokuwa na jamii yenye taarifa sahihi, tunakuwa na jamii yenye uwezo mkubwa wa kujikinga, kutoa taarifa mapema na kushiriki kikamilifu katika kuzuia na kudhibiti milipuko ya magonjwa," amesema.
Aidha, ameihakikishia UNICEF na wadau wengine kuwa Wizara ya Afya itahakikisha vifaa hivyo vinatunzwa na kutumika ipasavyo kwa madhumuni yaliyokusudiwa ili viweze kuleta matokeo chanya katika kuimarisha mawasiliano ya hatari na ushirikishwaji wa jamii, hususan katika ngazi za mikoa na halmashauri.
Kaimu Mkurugenzi Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Otilia Gowelle amesema vifaa hivyo vitakuwa na mchango mkubwa katika eneo la Kinga na kuimarisha Afya ya Mtanzania
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Rahma Hingora, amesema vifaa hivyo vitasaidia kutatua changamoto za mawasiliano katika utoaji wa elimu ya afya wakati wa majanga na milipuko ya magonjwa .
Naye Mwakilishi kutoka UNICEF nchini Tanzania, Bi. Ophilia Karumuna, amesema vifaa hivyo vitawawezesha wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi kwa kuwapatia taarifa sahihi kwa wakati.
Pia ameipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya kwa juhudi kubwa inazoendelea kufanyika katika kuboresha huduma za afya na kuimarisha kinga dhidi ya magonjwa, akieleza kuwa UNICEF itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha afya na ustawi wa wananchi.