Wizara ya Afya, kupitia Idara ya Huduma za Kinga, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO), imeandaa mafunzo ya Uelewa wa Tabia (Behavioural Insight) kwa Waratibu wa Elimu na Hamasa ya Afya pamoja na Waratibu wa Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kutoka mkoa wa Kigoma.
Akizungumza leo, tarehe 9 Julai 2026 mkoani Kigoma, Mratibu wa Mafunzo hayo, Bw. Simon Nzilibili kutoka Wizara ya Afya amesema mafunzo hayo yanalenga kuimarisha mbinu za uelimishaji na uhamasishaji wa jamii kuhusu huduma za uzazi wa mpango kwa kutumia ushahidi wa kitabia (Behavioural Insights). Mafunzo hayo yanafanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Maweni, Kigoma, kuanzia tarehe 9 hadi 15 Julai, 2026.
Washiriki wa mafunzo hayo ni Waratibu wa Elimu na Hamasa ya Afya, Waratibu wa Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto na Wasimamizi wa Uniti ya Uzazi, Mama na Mtoto katika Hospitali za Wilaya na ya Mkoa ndani ya Mkoa wa Kigoma
Ujengeaji uwezo kwa waratibu hawa unatarajiwa kuwawezesha kuwasaidia na kuwaongoza watoa huduma za afya katika kuboresha uhamasishaji wa huduma za uzazi wa mpango kwa kutumia mbinu zinazozingatia mwitiko wa tabia wa wateja, wagonjwa na jamii inayozunguka vituo vya kutolea huduma za afya. Hii itasaidia kuongeza matumizi ya huduma, kuboresha mawasiliano kati ya watoa huduma na wananchi, na kuimarisha utoaji wa huduma bora za afya ya uzazi, mama na mtoto.