Imeelezwa kuwa kuelewa vikwazo vinavyozuia wananchi kutumia huduma za uzazi wa mpango ni hatua muhimu katika kuboresha matumizi ya huduma hizo na kuimarisha afya ya uzazi, ya baba , mama na mtoto.
Akizungumza katika mwendelezo wa mafunzo ya Uelewa wa Tabia (Behavioral Insights) kwa Waratibu wa Elimu na Hamasa ya Afya katika Afya ya Uzazi, ya baba ,Mama na Mtoto mkoani Kigoma, Magdalena Dinawi kutoka Wizara ya Afya amesema kuwa ili kuboresha matumizi ya huduma za uzazi wa mpango ni muhimu kwanza kuelewa sababu zinazowafanya baadhi ya wananchi kutofika kupata huduma hizo.
Amesema kuwa kila mwananchi anaweza kuwa na sababu tofauti zinazomzuia kutumia huduma za uzazi wa mpango, hivyo ni muhimu kutambua vikwazo hivyo kabla ya kuandaa afua au kampeni za uhamasishaji.
Dinawi ameeleza kuwa miongoni mwa vikwazo vinavyojitokeza ni imani potofu kuhusu uzazi wa mpango, hofu ya madhara ya baadhi ya njia za uzazi wa mpango, mila na desturi, imani za kidini, ukosefu wa ushiriki wa wanaume katika maamuzi ya matumizi ya uzazi wa Mpango.
Aidha, amesema kuwa wakati mwingine wananchi wanaweza kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu huduma za uzazi wa mpango lakini wakashindwa kuzitumia kutokana na ukosefu wa motisha, ushawishi wa jamii au mazingira yasiyorahisisha kufikia huduma hizo.
Amesisitiza kuwa matumizi ya mbinu za Uelewa wa Tabia (Behavioral Insights) husaidia kubaini sababu halisi zinazowazuia wananchi kutumia huduma za afya, hivyo kuwezesha kubuni afua zinazolenga kuondoa vikwazo hivyo na kuongeza matumizi ya huduma za uzazi wa mpango.
Pia amewahimiza Waratibu wa Elimu na Hamasa ya Afya kuandaa kampeni na ujumbe unaozingatia mahitaji ya makundi mbalimbali ya jamii, ikiwemo wanawake wa umri wa kuzaa, wanaume, vijana balehe, viongozi wa dini na kimila pamoja na viongozi wa jamii, ili kujenga uelewa na kuondoa dhana potofu kuhusu uzazi wa mpango.
Mafunzo hayo yanaendelea mkoani Kigoma yakilenga kuwaimarisha Waratibu wa Elimu na Hamasa ya Afya katika kutumia mbinu za Uelewa wa Tabia ili kuongeza matumizi ya huduma za afya ya uzazi,ya baba , mama na mtoto, kuboresha utoaji wa elimu ya afya na kuleta mabadiliko chanya ya tabia katika jamii.