Na,Kanyuka Jonas, Kigoma.
Shirika la Enabel kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia limezindua darasa la kisasa lenye kuhamishika mkoani Kigoma, likiwa na lengo la kuwajengea walimu uwezo wa kutumia mbinu za kisasa za ufundishaji kupitia teknolojia, hatua inayotarajiwa kuongeza ubora wa elimu katika shule mbalimbali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isack Antony, ameipongeza Wizara ya Elimu na Shirika la Enabel kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu. Amesema uwekezaji huo unawawezesha walimu kupata maarifa mapya yanayokwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia, hivyo kuboresha kiwango cha ufundishaji na ujifunzaji.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Teknolojia kutoka Shirika la Enabel, Wolta John, amesema mradi huo unatekelezwa katika wilaya za Kibondo, Kasulu na Kigoma Ujiji. Ameeleza kuwa darasa hilo linatoa fursa kwa walimu kujifunza pamoja, kubadilishana uzoefu na kutumia teknolojia za kisasa ili kuongeza ufanisi katika ufundishaji darasani.
Naye Afisa Elimu wa Wilaya ya Kigoma Ujiji, Exavery Tambala, amesema kupitia mradi huo tayari yamepatikana mafanikio mbalimbali ikiwemo ujenzi wa mabweni, visima vya maji, matundu zaidi ya 40 ya vyoo, pamoja na upatikanaji wa kompyuta, vitabu na vifaa vingine vya kufundishia.
Amesema maboresho hayo yanachochea mazingira bora ya kujifunzia na kuongeza ufanisi wa walimu katika kutoa elimu.
Shirika la Enabel ni wakala wa maendeleo wa Serikali ya Ubelgiji unaotekeleza miradi ya maendeleo kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania. Kwa miaka kadhaa, shirika hilo limeendelea kufadhili na kutekeleza miradi katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, kilimo, maji na maendeleo ya jamii, kwa lengo la kuboresha huduma za kijamii na kuinua ustawi wa wananchi.