MAZOEZI YA MWILI, UZAZI WA MPANGO NI NGUZO MUHIMU ZA AFYA YA JAMII

MUUNGANO   MEDIA
0

 



Imeelezwa kuwa  utamaduni wa kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara pamoja na kutumia huduma za uzazi wa mpango, ni hatua ambazo  muhimu katika kuboresha afya ya mtu binafsi, familia na jamii kwa ujumla.

Akizungumza  tarehe 13 Julai,2026 wakati wa mwendelezo wa mafunzo ya Uelewa wa Tabia kwa Waratibu wa elimu na hamasa ya afya katika afya ya uzazi, mama na mtoto mkoani Kigoma yaliyoratibiwa na Wizara ya Afya, Idara ya Kinga, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kwa Kushirikiana na Shirika la Afya Duniani(WHO) Tanzania,  Anne Shuma kutoka Wizara ya Afya alisema kuwa mazoezi ya mwili husaidia kuimarisha afya ya moyo, kupunguza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza kama shinikizo la damu, kisukari na unene uliopitiliza, pamoja na kuboresha afya ya akili.



Ameeleza kuwa pamoja na umuhimu wa mazoezi, matumizi ya huduma za uzazi wa mpango yanawawezesha wanandoa kupanga idadi na nafasi ya watoto kulingana na uwezo wao wa kuwalea, jambo linalochangia afya bora ya mama na mtoto na ustawi wa familia.

Anne Shuma amebainisha kuwa bado zipo changamoto zinazochangia matumizi duni ya huduma za uzazi wa mpango katika baadhi ya maeneo, ikiwemo imani potofu za kimila na kidini, mfumo dume katika kufanya maamuzi ya kifamilia, pamoja na uelewa mdogo kuhusu faida za huduma hizo.

Amesitiza kuwa mbinu za Uelewa wa Tabia (Behavioral Insights) zina nafasi kubwa katika kubadili mitazamo na tabia zinazozuia wananchi kutumia huduma muhimu za afya. Aidha, alihimiza jamii kushiriki kikamilifu katika mazoezi ya mwili na kutumia huduma za uzazi wa mpango kwa ushauri .

Kwa upande wake, Mratibu wa Afya ya Mama na Mtoto kutoka Mkoa wa Kigoma .Benardetha Peter amesema baadhi ya changamoto zinazojitokeza katika suala la uzazi wa Mpango ni mfumo dume kwa jamii ambapo baadhi ya wanaume huamini kuwa suala la Afya ya Uzazi ni la Wanawake pekee.


 Wizara ya Afya inaendelea kuimarisha elimu kwa umma kupitia waratibu wa elimu na hamasa ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi zinazowasaidia kufanya maamuzi bora kuhusu afya zao.

Mwisho.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)