MATOKEO HASI YA AFYA HUTOKANA NA MTAZAMO WA TABIA.

MUUNGANO   MEDIA
0


Imeelezwa kuwa matokeo hasi ya afya katika jamii kwa kiasi kikubwa hutokana na mtazamo na tabia za watu kuhusu afya, hivyo kuna umuhimu wa kutumia mbinu za uelewa wa tabia ili kuwasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi yanayochangia kuboresha afya na ustawi wao.

Hayo yamejiri leo tarehe 11,Julai, 2026  katika Mafunzo ya Uelewa wa Tabia kwa Waratibu wa Elimu na Hamasa ya Afya katika Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto yaliyofanyika mkoani Kigoma, ambapo imebainika  kuwa tabia na maamuzi ya kila siku yana mchango mkubwa katika kuleta matokeo chanya au hasi ya afya.

Miongoni mwa mifano iliyotolewa ni kuchelewa kuanza huduma za kliniki kwa wajawazito, kutohudhuria huduma za kliniki kama ilivyopangwa, kutokujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya, kutowapeleka watoto kupata chanjo kwa wakati, kutotumia huduma za uzazi wa mpango pale zinapohitajika, kutonyonyesha watoto kwa kufuata miongozo ya kitaifa, pamoja na kutofuata ushauri wa wataalamu wa afya.

 Tabia hizo zinaweza kuathiri afya na ustawi wa mama, mtoto na familia kwa ujumla.

Aidha, imeelezwa kuwa tabia nyingine kama kutofanya mazoezi ya mwili mara kwa mara, kutokula lishe bora na mlo kamili, kutokuzingatia usafi wa mazingira na usafi binafsi, matumizi ya tumbaku na pombe kupita kiasi, kutoshiriki uchunguzi wa afya wa mara kwa mara, pamoja na kupuuza hatua za kinga zinazoshauriwa na wataalamu wa afya, zinaweza kuathiri afya na ustawi wa mtu binafsi, familia na jamii kwa ujumla.

 Simon Nzilibili kutoka Wizara ya afya akitoa  Mafunzo ya Uelewa wa Tabia kwa Waratibu wa Elimu na Hamasa ya Afya katika Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto yanayofanyika mkoani Kigoma.

Katika mafunzo hayo imesisitizwa kuwa mabadiliko ya tabia hayawezi kupatikana kwa kutoa taarifa pekee, bali yanahitaji kuelewa sababu zinazochochea maamuzi ya watu, mazingira wanayoishi, mila, desturi, imani na vichocheo vinavyoathiri tabia zao. Kwa kutumia mbinu za uelewa wa tabia, inawezekana kubaini vikwazo vinavyowazuia wananchi kutumia huduma za afya na kuandaa afua za mawasiliano zinazojibu mahitaji halisi ya jamii na kuhamasisha mabadiliko endelevu ya tabia.

Washiriki wamehimizwa kutumia maarifa na ujuzi walioupata katika mafunzo hayo kuandaa na kutekeleza afua za mawasiliano zinazozingatia uelewa wa tabia ili kuongeza matumizi ya huduma za afya, kuimarisha ushiriki wa jamii katika masuala ya afya na kuboresha matokeo ya afya ya uzazi, mama na mtoto pamoja na afya ya jamii kwa ujumla.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Wizara ya Afya, Idara ya Kinga, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani(WHO) kwa lengo la kuimarisha uwezo wa Waratibu wa Elimu na Hamasa ya Afya katika kutumia mbinu za uelewa wa tabia ili kuboresha utoaji na matumizi ya huduma za afya nchini.

Tags

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)