WAANDISHI WA HABARI WANAOCHOCHEA AGENDA YA HEDHI SALAMA WATUNUKIWA TUZO ZA MHH MEDIA AWARDS 2026

MUUNGANO   MEDIA
0

mwakilishi wa Watangazaji Anaitwa Mwanne Othman Mtangazaji wa kipindi cha Dadaz EATv alipewa Mwongozo akasambaze kwa waandishi wengine

Mohammed Hammie kutoka Michuzi Blog akipewa tuzo ya umahiri katika uandishi masuala ya elimu ya afya kuhusu hedhi salama.


Clara Tarimo kutoka Radio Free Africa akipewa tuzo ya umahiri katika uandishi masuala ya elimu ya afya kuhusu hedhi salama.

Anitha Damson kutoka Highland fm akipewa tuzo ya umahiri katika uandishi masuala ya elimu ya afya kuhusu hedhi salama.



Herieth Makweta kutoka Gazeti la Mwananchi akipatiwa tuzo ya umahiri katika masuala ya uandishi elimu ya afya kuhusu hedhi salama.

Na.Faustine Gimu, Elimu ya Afya,Dodoma

Waandishi wa habari na wadau wa vyombo vya habari walioonesha umahiri katika kuandika na kuripoti masuala ya hedhi salama nchini wametunukiwa tuzo mbalimbali za MHH Media Awards 2026, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao katika kuelimisha jamii na kuhamasisha utekelezaji wa afua za hedhi salama kwa wasichana na wanawake nchini.

Akizungumza wakati wa kutangaza washindi wa tuzo hizo Jijini Dodoma Katibu wa Jukwaa la Hedhi Salama Tanzania (Menstrual Health and Hygiene Coalition), Severine Allute, amesema kuwa tuzo hizo zimeanzishwa kwa lengo la kuhamasisha na kutambua mchango wa waandishi wa habari wanaotumia kalamu, sauti na picha kuibua mijadala chanya kuhusu hedhi salama na kuondoa unyanyapaa unaohusiana na suala hilo.

Amesema tangu kuanzishwa kwa tuzo hizo, kumekuwa na ongezeko kubwa la habari, vipindi na makala zinazohusu hedhi salama katika vyombo mbalimbali vya habari, jambo ambalo limechangia kuimarika kwa uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa hedhi salama kwa afya, elimu na ustawi wa wasichana na wanawake.

“Vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuelimisha jamii, kubadilisha mitazamo hasi, kuondoa dhana potofu na kuhamasisha mabadiliko ya tabia. Kutokana na mchango huo mkubwa, Jukwaa la Hedhi Salama Tanzania limeendelea kutumia tuzo hizi kama njia ya kuwapongeza na kuwahamasisha waandishi wa habari kuendelea kuipa uzito agenda ya hedhi salama,” amesema Allute.

Ameongeza kuwa kupitia kazi za waandishi wa habari, jamii imeendelea kupata uelewa kuhusu changamoto zinazowakabili wasichana na wanawake wakati wa hedhi pamoja na umuhimu wa kuhakikisha upatikanaji wa huduma rafiki, elimu sahihi, bidhaa salama za hedhi na miundombinu wezeshi katika shule, maeneo ya kazi na jamii kwa ujumla.

Katika tuzo za mwaka 2026, washindi walitoka katika makundi manne ambayo ni Redio, Televisheni, Magazeti na Blogu.

Washindi wa kundi la Redio walikuwa ni Anitha Damson wa Highlands FM, Clara Tarimo wa RFA Radio na Samwel Mussa wa Highlands FM Radio. Katika kundi la Televisheni, washindi walikuwa ni Kisali Simba wa Star TV na Faraja Sendegeya wa Azam TV.

Kwa upande wa magazeti, washindi walikuwa ni Najjat Omary wa Majira Newspaper na Herieth Makwetta, huku katika kundi la Blogu mshindi alikuwa ni Mohammed Hammie wa Michuzi Blog.

Jukwaa la Hedhi Salama Tanzania limeeleza kuwa litaendelea kushirikiana na vyombo vya habari nchini ili kuhakikisha agenda ya hedhi salama inaendelea kupewa kipaumbele, kwa lengo la kujenga jamii yenye uelewa, usawa na mazingira salama kwa wasichana na wanawake wote nchini.

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)