VIONGOZI NA WADAU WAHIMIZWA KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA KUBORESHA HUDUMA ZA HEDHI SALAMA NCHINI.

MUUNGANO   MEDIA
0




Katika juhudi za Serikali za kuendelea kuimarisha afya, ustawi na maendeleo ya wasichana na wanawake nchini,Jamii na  wadau mbalimbali wametakiwa kuongeza ushirikiano na uwekezaji katika afua za hedhi salama ili kuhakikisha kila msichana na mwanamke anapata elimu sahihi, huduma rafiki, bidhaa salama za hedhi pamoja na mazingira wezeshi yanayolinda afya, heshima na utu wake.


 Hatua hiyo inalenga kuondoa changamoto zinazowakabili wasichana na wanawake wakati wa hedhi ambazo wakati mwingine huathiri mahudhurio shuleni, ushiriki katika shughuli za kijamii na kiuchumi pamoja na kujiamini kwao katika jamii.

Hayo yamesemwa Jijini Dodoma na Mwakilishi wa Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Afya   Dkt. Saitore Laizer, wakati akifungua Kikao cha Kitaifa cha Uraghibishi wa Afua za Hedhi Salama Nchini kikao kilichowakutanisha viongozi waandamizi kutoka Wizara mbalimbali, taasisi za Serikali, mashirika ya maendeleo, sekta binafsi, asasi za kiraia, Jukwaa la hedhi Salama ,wataalamu wa afya pamoja na wadau wengine wanaojihusisha na masuala ya hedhi salama nchini.


Dkt. Laizer amesema kuwa hedhi ni hali ya kawaida ya kibaiolojia inayowapata wasichana na wanawake, hivyo ni muhimu jamii ikajenga mazingira yanayowezesha suala hilo kusimamiwa kwa usalama, heshima na staha bila kuwepo kwa unyanyapaa, dhana potofu au vikwazo vinavyoweza kuathiri ustawi wa wanawake na wasichana.

Ameeleza kuwa pamoja na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali na wadau, bado kuna changamoto zinazohitaji nguvu ya pamoja ikiwemo ukosefu wa elimu sahihi kuhusu hedhi, upatikanaji hafifu wa bidhaa salama za hedhi kwa baadhi ya makundi, pamoja na changamoto za miundombinu ya maji, usafi na mazingira katika baadhi ya shule, taasisi na maeneo ya umma.

Aidha, amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tayari imeandaa Mwongozo wa Hedhi Salama na Zana zake wa mwaka 2025 ambao unaelekeza namna bora ya utekelezaji wa afua za hedhi salama nchini. Mwongozo huo umebainisha maeneo muhimu ya kupewa kipaumbele ikiwemo utoaji wa elimu kwa jamii, ujenzi wa miundombinu rafiki kwa wasichana na wanawake, uzalishaji na usambazaji wa bidhaa za hedhi zenye ubora uliothibitishwa pamoja na kuimarisha uratibu wa wadau katika utekelezaji wa afua hizo.

Dkt. Laizer amesisitiza kuwa mafanikio ya afua za hedhi salama hayawezi kupatikana kwa juhudi za Serikali pekee, bali yanahitaji ushiriki wa wadau wote wakiwemo viongozi wa dini, wazazi, walimu, sekta binafsi, mashirika ya maendeleo, vyombo vya habari na jamii kwa ujumla katika kujenga uelewa na kuondoa vikwazo vinavyowakabili wasichana na wanawake wakati wa hedhi.


Ameongeza kuwa hedhi salama si suala la afya pekee, bali ni ajenda mtambuka inayohusu elimu, maendeleo ya kijamii, uchumi na haki za binadamu. Hivyo, uwekezaji katika afua za hedhi salama ni uwekezaji katika maendeleo ya taifa kwa kuwa unachangia kuwawezesha wasichana na wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo bila kukwamishwa na changamoto zinazohusiana na hedhi.

Akihitimisha, Dkt. Laizer amewataka washiriki wa kikao hicho kutumia fursa hiyo kujadili kwa kina na kuazimia mikakati madhubuti ya kuimarisha utekelezaji wa afua za hedhi salama nchini ili kufikia malengo yaliyowekwa katika mwongozo wa taifa wa hedhi salama.

"Ni wajibu wetu sote kuhakikisha kuwa kila msichana na mwanamke anaishi kwa heshima, usalama na kujiamini wakati wa hedhi.

" Hedhi si laana, si uchafu na si jambo la kuogopwa, bali ni sehemu ya kawaida ya maisha na afya ya mwanamke. Tukimuwezesha mwanamke na msichana kuwa salama wakati wa hedhi, tunachangia kujenga jamii yenye afya, usawa na maendeleo endelevu," amesisitiza Dkt. Laizer.

Wizara za Kisekta zilizohudhuria Kikao hiki cha ni Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu, Wizara ya Afya ,Wizara ya Maji,Wizara Elimu Sayansi ya Teknolojia,Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi maalumu ,Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Fedha.

Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)