Na Avelina Musa - DODOMA.
Waziri wa Nishati, Mhe.Deogratius Ndejembi, amesema Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imeendelea kusimamia mradi wa uzalishaji umeme wa Julius Nyerere (JNHPP - MW 2,115) wa kimkakati, ambao tayari umekamilika na umeme unaendelea kuzalishwa kupitia mitambo yote tisa ya uzalishaji kwa kuzingatia mahitaji ya umeme.
Mhe.Ndejembi amesema hayo leo Aprili 22, 2026 bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Ndejembi amesema mbali na usimamizi wa mradi huo, kazi nyingine zilizofanyika ni pamoja na kufanya marekebisho madogo madogo (snags rectification) na kukamilisha ujenzi wa ghala la kuhifadhia vifaa katika kituo cha kupoza umeme cha Chalinze.
Amesema TANESCO na Bodi ya Bonde la Mto Rufiji imeingia makubaliano ya ushirikiano katika kutunza vyanzo vya maji na ushirikishwaji wa wadau katika utunzaji wa vyanzo vya maji yanayoelekea katika mradi.
Aidha amesema kazi nyingine zilizofanyika katika mradi huo ni kukamilisha zoezi la udabuaji wa mto Mswiswi wenye urefu wa kilomita 29 na kufanya tathmini ya maeneo ya kupanda miti kwenye madakio (catchment) ya bonde la mto Rufiji ambapo jumla ya miti 5,000 imepandwa katika maeneo ya Wanging'ombe, Kidatu, Kihansi na Mtera.
"Serikali imefanya zoezi la kufunga mifereji isiyo rasmi katika maeneo ya Wanging'ombe, Kilombero, Mbarali, Ifakara, Iringa, Mahenge na Kilosa na kukamilisha ujenzi wa tuta"amesema.
Hata hivyo ameongeza kuwa Serikali imefanya zoezi la kufunga mifereji isiyo rasmi katika maeneo ya Wanging'ombe, Kilombero, Mbarali, Ifakara, Iringa, Mahenge na Kilosa na kukamilisha ujenzi wa tuta lenye urefu wa kilomita 11 la kuzuia mafuriko na upotevu wa maji kwenye mto Lumemo katika eneo la Ifakara.
Mwisho.
