Na Avelina Musa - DODOMA.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi asilia Dkt. James Mataragio, ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (Petroleum Upstream Regulatory Authority - PURA) kwa usimamizi wa miradi ya mafuta na gesi asilia huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya utekelezaji ili kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.
Mataragio ametoa pongezi hizo leo Aprili 21, 2026 mara baada ya kupokea maelezo ya utekelezaji wa mradi huo alipotembelea banda la PURA katika Maonesho ya Wiki ya Nishati yanayoendelea katika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma.
Akiwa kwenye banda hilo, Dkt Mataragio alipata ufafanuzi kuhusu maendeleo ya miradi ya utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia katika maeneo ya Lindi na Mtwara, hususani mradi wa uchorongaji visima katika kitalu cha Mnazi Bay.
Akitoa taarifa kwa Dkt. Mataragio, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau kutoka PURA, Bw. Charles Nyangi amesema tayari kisima kimoja kati ya vitatu kimeshachimbwa na uchimbaji wa kisima cha pili unaendelea.
Bw.Charles amesema kupitia usimamizi wa PURA, uchimbaji wa kisima cha kwanza (MB5) umekamilika kwa wakati na kwa mafanikio makubwa ambapo Kisima hicho kimeshafanyiwa majaribio na kuingizwa katika uzalishaji ambapo kina uwezo wa kuzalisha wastani wa futi za ujazo milioni 40 kwa siku.
"Kiasi hicho kimeongeza uzalishaji wa gesi asilia kutoka Kitalu cha Mnazi Bay kutoka wastani wa futi za ujazo milioni 90 kwa siku hadi kufikia wastani wa futi za ujazo milioni 130 kwa siku" amesema Nyangi.
Aidha amesema PURA imeendelea na usimamizi wa uchimbaji wa kisima cha pili (MS-2) ambapo kazi inaendelea vizuri ambapo hadi kufikia Aprili 20, 2026, zaidi ya mita 1400 zilikuwa zimeshachimbwa.



