EWURA YATUMIA WIKI YA NISHATI KUELIMISHA WADAU.

MUUNGANO   MEDIA
0

 ‎


Na Avelina Musa - DODOMA.


Kaimu Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Wilfred Mwakalosi amesema EWURA imetumia fursa ya Wiki ya Nishati kuelimisha wadau kuhusu namna inavyohakikisha upatikanaji wa huduma za nishati na maji kwa wakati na kwa gharama nafuu.


Mwakalosi amesema hayo leo Aprili 21, 2026 katika maonesho ya wiki ya Nishati Jijini Dodoma ambapo amesema wanatumia fursa hiyo kuwahamasisha wabunge kuwekeza katika ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini pamoja na vituo vya gesi asili kwa ajili ya magari (Compressed Natural Gas - CNG) ili kusogeza huduma kwa wananchi.


 Amesema wabunge ni wawakilishi wa wananchi, hivyo kuwajengea uelewa kuhusu udhibiti, fursa za uwekezaji na utaratibu wa kushughulikia migogoro na malalamiko kutawawezesha kuwasilisha taarifa sahihi kuhusu juhudi za Serikali katika kuhakikisha huduma bora za umeme, mafuta na gesi asilia.


Kwa upande wake, Mchumi wa EWURA Bi. Achilana Mtingele,amesema elimu inayotolewa imejikita katika kueleza namna EWURA inavyosimamia upangaji wa viwango vya bei za huduma za umeme, mafuta na gesi asilia.



"EWURA huweka mizania kati ya maslahi ya watoa huduma na watumiaji, na wabunge waliopata elimu hiyo wataweza kuiwasilisha ipasavyo kwa wananchi katika maeneo yao."Amesema.


 Aidha Ofisa Mwandamizi wa Kitengo cha Mafuta, Ibrahim Kajugusi, amesema elimu inayotolewa inalenga kuwafahamisha wananchi jinsi EWURA inavyosimamia upatikanaji wa huduma za mafuta kwa kuzingatia ubora na gharama sahihi. 



Kwa upande wa sekta ya umeme, Mhandisi Mwandamizi wa Umeme, Lulu Chilumba, amewahamasisha wabunge na wadau wanaotembelea maonesho hayo kutumia mafundi umeme wenye leseni kutoka EWURA ili kuhakikisha usalama wa nyumba na mali zao. 


" EWURA inaendelea kutoa leseni kwa mafundi umeme wenye sifa stahiki, ambapo zaidi ya leseni 1,000 zilitolewa katika mwaka wa fedha uliopita."amesema.


Akizungumzia sekta ya gesi asilia, Mhandisi Mwandamizi wa Gesi Asilia, Mhandisi Evaline Rweikiza, amesema EWURA itaendelea kusimamia ubora wa miundombinu ya gesi asilia nchini na kuhamasisha matumizi yake, hususan katika magari.


Amesema hadi sasa vituo 18 vimepata leseni ya EWURA kutoa huduma ya gesi asilia, huku vituo sita vingine vikiwa katika hatua za mwisho za kupata leseni katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ambapo mipango inaendelea kwa baadhi ya makampuni kusambaza gesi asilia iliyokandamizwa katika Mikoa ya Morogoro na Dodoma.


Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)