Na Avelina Musa - Dodoma.
Katibu wa NEC,Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) CPA Amos Makalla amesema kikao cha mwisho cha uteuzi watia nia walioomba kugombea nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) sasa kufanyika Julai 28 mwaka huu.
Amesema kikao hicho kitatanguliwa na Kikao cha Kamati Kuu ya CCM kisha kufuatiwa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM vitakavyofanyika Julai 26 mwaka huu.
CPA Makala amesema hayo leo Julai 19,2025 Jijini Dodoma,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mchakato wa uteuzi na mabadiliko ya tarehe ya kikao.
Amesema wagombea ni wengi, kazi kubwa imefanyika kwani tunataka haki itendeke kwa kufanya uteuzi makini, hivyo tumejipa nafasi mpaka tarehe 28.
CPA Makala amesema CCM ni Chama makini chenye uzoefu na baada ya uteuzi kukamilika ratiba kuhusu kura za maoni itatolewa rasmi.
"Mpaka sasa hakuna mgombea aliyekatwa katika mchakato wa uteuzi kama ambavyo baadhi ya watu wanavyodai."Amesisitiza CPA Makala.
"Taratibu za Chama zinaeleweka kwani vikao vya mwisho vya uteuzi bado havijafanyika. Ndiyo maana wakati wa kuchukua fomu tukakataza watia nia wasije na matarumbeta maana watu wataanza kuhoji nani aliyekuja na matarumbeta au wapambe wengi."Amesema.
Aidha vikao hivyo vilipangwa kufanyika jana na leo ambapo majina matatu yalitarajiwa kupitishwa katika kila nafasi kisha wanachama kuyapigia kura za maoni.
Amesema chama hicho kimeamua kuongeza muda ili kuhakikisha kila hatua ya uchambuzi inafanyika kwa makini na kwa kuzingatia vigezo, huku akiwataka wagombea kuwa watulivu wakati mchakato huo ukiendelea.
Mwisho.
.jpg)