Wito huu umetolewa Julai 21, 2025 na Polisi Kata ya Mahenje Mkaguzi wa Polisi Nelson Mwinuka wakati alipokuwa anacheza mchezo wa bao na wazee hao katika Kijiji cha Mahenje Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe na kuwataka wazee hao kuwa mabalozi wa kutangaza amani ili jamii iendelee kuwa salama.
Mkaguzi Mwinuka akizungumza na wazee hao alisema amani ni msingi wa maendeleo aliwaomba wazee hao kuwa na wajibu wa kuishauri jamii na kuzuia migogoro kabla haijatokea na kujua umuhimu wa utamaduni wa mazungumzo ya maridhiano katika kutatua changamoto katika jamii kitendo ambacho kitaleta maendeleo katika jamii husika.
“Tumieni ushawishi wenu kushirikiana na taasisi za dini katika kuendelea kuelimisha jamii kuhusu amani kwa vijana na makundi mengine kama Jeshi la Polisi linavyofanya, huku akiwasisitiza kuwa maadili, busara na hekima yao vina mchango mkubwa katika kudumisha utulivu, hasa nyakati za uchaguzi au migogoro ya kifamilia na kijamii.
Mwisho, Mkaguzi Mwinuka alihitimisha kwa kuwaomba wazee hao kushirikiana na wadau mbalimbali ili waweze kuwa daraja kati ya kizazi kipya na historia ya jamii, wakiongoza kwa mfano na kuhakikisha kuwa ujumbe wa amani unapenya kila kona ya taifa ili jamii iendelee kuwa salama.
