Hayo yamebainishwa leo Julai 18, 2025 na Afisa Afya Mazingira Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Bw. Sasita Shabani wakati wa kufunga mafunzo hayo rasmi yaliyofanyika kwa siku tatu mkoani Morogoro.
Amesema wataalam hao wanatakiwa kuzingatia lengo la mafunzo hayo
na kutimiza wajibu wao wa kulinda afya za wananchi hasa kwenye maji ambayo ndiyo msingi mkubwa kwenye maisha ya kila siku.
Kwa upande wake Mkuu wa Sehemu ya Chakula Salama, Maji Salama na Usafi wa Mazingira kutoka Wizara ya Afya, Bw. Anyitike Mwakitalima, amewaasa wataalam wa afya waliopata mafunzo ya jinsi ya kupima na kugundua sampuli za maji kuhakikisha wanatumia elimu hiyo kwa vitendo katika maeneo yao ya kazi ili kutimiza lengo la Serikali la kutoa mafunzo hayo.
"Tunatoa mafunzo haya si kwa ajili ya kumbukumbu tu au kujaza ripoti, bali kwa ajili ya utekelezaji tukirudi ofisini. Ni muhimu wataalam mliopata ujuzi huu kuhakikisha mnayatumia maarifa haya kwa ukamilifu katika maeneo yenu, kwa kupima sampuli za maji mara kwa mara na kuwasilisha taarifa sahihi zitakazosaidia kuzuia magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji machafu. Afya ya wananchi ipo mikononi mwenu," amesema Bw. Mwakitalima.
Naye, Afisa Afya Mazingira mkuu Wizara ya Afya Mariam Mashimba, amewasihi wataalam waliopata mafunzo hayo kujua umuhimu wa kuandaa ripoti ambayo itasaidia wakati wa uchukuaji sampuli kwa kuhusisha vyanzo vyote vya maji vitakavyochukuliwa eneo husika ili kugundua kata zinazotumia vyanzo vya maji visivyo salama na idadi ya watu wanaoathirika kwa takwimu sahihi.
“Ripoti nzuri ya uchunguzi wa vyanzo vya maji ni msingi wa kufanya maamuzi sahihi, hivyo tunawataka wataalam wote waliopata mafunzo haya kuhakikisha wanajumuisha taarifa kutoka vyanzo vyote vya maji wanavyovikagua, ili iwe rahisi kubaini maeneo yanayokabiliwa na changamoto ya maji salama pamoja na idadi ya wananchi walio hatarini," amesema Bi. Mashimba.
Amesema pia ripoti hizo zitasaidia kupanga hatua stahiki kwa mujibu wa takwimu halisi.
Kwa upande wake Mteknolojia Maabara Hospitali ya Rufaa Morogoro Herieth Goodluck ambaye pia ni mnufaika wa mafunzo hayo, amewakumbusha wataalam wa afya kutumia nyenzo za kujilinda kama barakoa, glovu na viatu vya maji wanapokwenda kuchukua sampuli ili kujiepusha na magonjwa yanayoweza kutokea wakati wanapotimiza majukumu yao.
