UCHUMI WA MKOA WA MARA WAENDELEA KUIMARIKA MIAKA MINNE YA RAIS DKT.SAMIA-RC MTAMBI.

MUUNGANO   MEDIA
0

 




Na Avelina Musa - Dodoma.


Katika kipindi cha Miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita,Uchumi wa Mkoa wa Mara umeendelea kuimarika ambapo pato halisi limeongezeka kutoka shilingi trilioni 5.3 mwaka 2020 hadi trilioni 6.8 mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 28.3 kwa mwaka ambapo Hadi kufikia  Juni 30, 2025 shilingi trilioni 1.3 zimetolewa na Mhe. Rais Samia kwa ajili ya kutekeleza miradi katika sekta mbalimbali katika Mkoa wa Mara.


Miradi mikubwa ya maji mkoani humo ni pamoja na mradi wa Mgango -Kiabakari- Butiama wenye thamani ya shilingi bilioni 70.5 ambao umekamilika, Rorya-Tarime wenye thamani ya shilingi bilioni 134.4 ambao umeanza kutekelezwa na mradi wa Mji wa Mugumu wenye thamani ya dola za marekani milioni 8.75 ambao umeanza kutekelezwa. 

  

 Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe.Kanali Evans Alfred  Mtambi  wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya Sita Julai  18 Jijini Dodoma ambapo amesema Serikali inatekeleza miradi ya majitaka miwili ambapo imechimba mabwawa ya kusafishia maji taka katika Manispaa ya Musoma wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 33 na mradi wa majitaka wa Butakale katika Mji wa Bunda wenye thamani ya shilingi bilioni 1.728 ambao unaendelea kutekelezwa.

Mhe.Mtambi amesema Serikali imefanya uwekezaji katika miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji wa mpunga katika Kijiji cha Mariwanda, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwa gharama ya shilingi milioni 213.05. Aidha, imejenga miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji wa mpunga katika Kata ya Rabour, Wilaya ya Rorya kwa gharama ya shilingi milioni 982.82.


"Serikali imekusanya maduhuli ya shilingi bilioni 568 kutokana na malipo ya mrahaba, ada ya ukaguzi kwenye mauzo ya madini, ada za leseni na tozo mbalimbali za vibali, ushuru wa huduma katika Halmashauri na kodi ya zuio inayokatwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania."Amesema 


Aidha katika Sekta ya Madini kuna urudishwaji wa faida kwa jamii kutoka kwa wamiliki wa leseni na kampuni za uchimbaji madini (CSR). Kwa miaka hii minne kumekuwa na utekelezaji wa miradi 398 ya huduma za jamii yenye thamani ya shilingi bilioni 33.81 zitokanazo na CSR ya sekta ya madini.

"Katika kipindi hiki Serikali imeboresha majengo ya utawala kwa ajili ya kuboresha mazingira ya utoaji huduma kwa wananchi. Majengo yaliyojengwa ni Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama, majengo ya utawala ya Halmashauri sita yamekamilika na ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti umeanza katika mwaka wa fedha 2025/2026 na unaendelea"

Amesema Serikali imenunua magari ya viongozi ikiwa ni pamoja na gari la Mkuu wa Mkoa, magari ya Wakuu wa Wilaya zote sita na magari kwa ajili ya Idara na Vitengo vya Sekretarieti ya Mkoa wa Mara.

"Katika kipindi hiki, majengo ya ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Butiama, Ofisi ya Uhamiaji Wilaya ya Butiama yamejengwa"


"Ujenzi wa majengo haya ya utawala umeboresha mazingira ya kutolea huduma kwa wananchi, mazingira ya kufanyia kazi kwa watumishi na mandhari ya maeneo hayo"

Hata hivyo amesema  Mkoa wa Mara ni kati ya mikoa yenye utajiri mkubwa wa madini ikiwemo dhahabu, fedha, shaba, chuma, madini ya ujenzi, madini ya viwandani na madini ya vito. Madini ya dhahabu ndio yanayochimbwa kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na madini mengine.

Amesema hadi kufikia Juni, 2025 Mkoa ulikuwa na lesseni 2,288 ambazo zinahusisha uchimbaji wa madini, utafiti, uchenjuaji na biashara ya madini.

Aidha, Mkoa kwa kushirikiana na Tume ya Madini na Mgodi wa Barrick North Mara umewawezesha upatikanaji wa lesseni 104 kwa vikundi 48 vyenye jumla ya Vijana 1,836 kutoka vijiji 13 katika eneo la Nyamongo, Wilaya ya Tarime.

"Uwezeshaji wa makundi hayo ni semehu ya utekelezaji wa programu ya Mining for a Brighter Tomorrow (MBT) na una lengo la kutoa fursa kwa vijana kushiriki katika mnyororo wa thamani wa madini"

"Vijana hao wanapatiwa elimu kuhusu uchimbaji wa madini chini ya uangalizi wa Mgodi wa Barrick North Mara, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Ofisi ya Madini Mkoa"Amesisitiza

Serikali imetoa miongozo ya kuyawezesha makundi mbalimbali katika jamii kuweza kuimarisha uwezo wao wa kushiriki shughuli za maendeleo na kuleta usawa wa kiuchumi katika jamii.

"Katika kipindi hiki, kuna ongezeko la vikundi vinavyonufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri za Mkoa wa Mara kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutoka vikundi 187 mwezi Novemba, 2020 hadi vikundi 324 Aprili, 2025"Amesema Mhe.Mtambi.





Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)