TUWEKE MIKAKATI YA PAMOJA KATIKA KUHAKIKISHA KILA MTANZANIA ANATUMIA MAJI SAFI NA SALAMA KUJIKINGA NA MAGONJWA YA MLIPUKO-DKT.MMBAGA.

MUUNGANO   MEDIA
0

 

Wataalam wa Afya Mazingira wa Halmashauri wamehimizwa kuendelea kuweka mikakati ya pamoja katika kuhakikisha kila mtanzania ana uelewa sahihi juu ya umuhimu wa matumizi sahihi ya maji safi na salama katika kujikinga na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu.


Wito huo umetolewa leo tarehe 16,Julai, 2025 Mkoani Morogoro na Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Epidemiolojia na Udhibiti wa Magonjwa kutoka Wizara ya Afya Dkt. Vida Mmbaga akimwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali katika Ufunguzi wa Mafunzo ya Ufuatiliaji Ubora wa Maji ya Kunywa Ngazi ya Kaya kwa Wataalam wa Afya Mazingira kutoka Halmashauri mbalimbali nchini.


Dkt. Mmbaga amesema ni muhimu kwa kila mmoja kuweka mikakati ya Kinga dhidi ya magonjwa ya mlipuko.


“Tunapoweka ya Kinga tunazuia magonjwa mengine , hivyo ni muhimu kuhakikisha jamii inatambua umuhimu wa maji safi na salama na kuhakikisha inakuwa na desturi ya kunawa mikono mara kwa mara kwenye mikusanyiko ya watu”amesema.


Aidha, Dkt. Mmbaga amesema takwimu zinaonesha kuwa upatikanaji wa maji safi ya kunywa pamoja na hali ya vyoo bora unapofikia au unapozidi asilimia 75 uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu ni nadra kutokea.


“Kutokana na Umuhimu wa matumizi ya maji safi na salama ya kunywa, Wizara ya Afya imeona umuhimu kuandaa na kuendesha mafunzo ya upimaji na ufuatiliaji wa usalama wa maji ya kunywa .HAtua hii inalenga kujengea uwezo Mikoa na Halmashauri katika kubaini viashiria vya uchafuzi wa maji na kuchukua hatua stahiki kabla ya kutokea kwa mlipuko na hii ndio dhana ya Kinga ni Bora kuliko Tiba na hivyo tunataka kuona hatua za kuzuia milipuko zinachukuliwa mapema na kwa kiwango cha kutosheleza kwani upatikanaji wa maji safi ya kunywa pamoja na hali ya vyoo bora unapofikia 75% ni nadra kutokea kwa Kipindupindu”amesema.


Kwa upande wake ,Mkuu wa Sehemu ya Chakula Salama, Maji Salama na Usafi wa Mazingira kutoka Wizara ya Afya Bw.Anyitike Mwakitalima amesema lengo la Mafunzo hayo ni kuhakikisha kila mtaalamu wa Halmashauri anakuwa na uelewa namna ya upimaji wa Maji ya Kunywa katika kujikinga na Magonjwa ya mlipuko.


Kwa upande wao baadhi ya wanufaika wa Mafunzo hayo akiwemo Afisa Afya Mazingira kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara Bw. Said Ame pamoja na Afisa Afya Mazingira Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga wamesema kupitia mafunzo hayo yatarahisisha kuchukua hatua za mapema katika kujikinga na magonjwa ya mlipuko .


Halikadhalika Dkt. Mmbaga amezipongeza Halmashauri zilizonunua Vifaa hivyo ambazo ni 70 kati ya 184 na kuzielekeza zilizobaki kufanya hivyo.


Wataalam wa Afya Mazingira Ngazi ya Mikoa na Halmashauri waliohudhurika katika mafunzo hayo ni kutoka Mikoa ya Pwani, Mwanza, Simiyu, Geita, Singida, Morogoro, Lindi, Ruvuma, Songwe, Iringa, Rukwa, Tanga, Mtwara na Manyara.














Chapisha Maoni

0Maoni
Chapisha Maoni (0)