Na Avelina Musa - Dodoma.
KATIKA Kipindi cha Uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassani Mkoa wa Katavi kupitia Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) umepokea jumla ya Shilingi 33,529,634,479.08 (Bilioni 33.352) kwa ajili ya miradi 51 ya Maji vijijini.
Utekelezaji wa miradi hii imesaidia kuongeza idadi ya watumiaji wa Maji vijijini kutoka asilimia 62.2 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 77.3 Juni, 2025 sawa na ongezeko la asilimia 15.1.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Hoza wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya Sita leo Julai 03.2025 Jijini Dodoma.
Mhe.Mwanamvua amesema Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mpanda (MUWASA) inatoa huduma ya Maji katika Kata 15 za Manispaa ya Mpanda ambapo katika kipindi cha uongozi wa Rais wa awamu ya Sita, Mkoa umeendelea kutekeleza miradi MITANO yenye thamani ya Shilingi bilioni 32,163,080,399.89 ambayo ikikamilika itaongeza upatikanaji wa Maji kwa zaidi ya asilimia 100.
"Mkoa unaendelea kutekeleza mradi wa usamabazaji Maji kutoka Bwawa la Milala unaotekelezwa chini ya mpango wa ujenzi wa mradi wa Maji wa Miji 28,Mradi huu unatarajiwa kuzalisha Maji lita 12,000,000 kwa siku na kunufaisha wakazi wote wa Manispaa ya Mpanda, Hadi kufikia Juni, 2025 hatua ya utekelezaji imefikia asilimia 42 mradi unatekelezwa kwa muda wa miezi 30 kuanzia 11 Aprili, 2023 na unatarajiwa kukamilika Mwezi Oktoba 2025"
Kwa upande wa sekta ya kilimo, Mhe.Mwanamvua amesema ukarabati wa skimu kubwa za umwagiliaji za Mwamkulu na Kabage unaendelea kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 55, na tayari utekelezaji wake umefikia hatua ya robo.
"Kukamilika kwake kutasaidia kuongeza eneo la umwagiliaji mara zaidi ya mbili, na kuongeza uzalishaji wa mpunga kwa kiwango kikubwa. Vilevile, vijana zaidi ya mia saba wamepatiwa mafunzo ya kilimo cha kisasa, huku vyama vya ushirika vikiendelea kuongezeka kwa kasi."Amesema.
Aidha katika sekta ya afya amesema Zahanati zimeongezeka kutoka 80 mwaka 2021 hadi 127 mwaka 2025 sawa na ongezeko la zahanati 47, Vituo vya Afya vimeongezeka kutoka 17 mwaka 2021 hadi kufikia 28 mwaka 2025 sawa na ongezeko la vituo 11 sawa na ongezeko la asilimia 39 pamoja na Ukamilishaji wa Hospitali 4 za Wilaya na ukarabati wa hospitali Kongwe ya Manispa ya Mpanda umekamilika.
"Ujenzi wa jengo la ‘Dialysis” (Huduma ya kusafisha Damu) umekamilika kwa asilimia 100 na huduma zimeanza kutolewa, Ujenzi wa jengo la huduma za dharura (EMD), Ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi (ICU), Ujenzi wa nyumba ya mtumishi,Ununuzi wa mashine ya CT-Scan, Ununuzi wa mashine mbili za kisasa za mionzi (digital X-Ray) pamoja na Ununuzi wa Vifaa tiba mbalimbali".
"Mafanikio makubwa ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ni wananchi kupata huduma kirahisi, kupunguza kusafirisha wagonjwa kwenda nje kwa kuendelea kupata huduma za ki-bingwa ambazo ni Huduma za kibigwa za upasuaji, Huduma za kibingwa za mifupa, Huduma za kibingwa za afya ya uzazi, Huduma za kibingwa za sikio, pua na kinywa, huduma za kibingwa za Magonjwa ya Ndani pamoja na huduma za kibingwa za magonjwa ya dharura".
Amesema Mwaka 2021 Mkoa ulipokea kiasi cha Tshs 2,980,556,000.00 za ununuzi wa dawa, Vifaa, Vifaa tiba na vitendanishi na kwa mwaka 2024 mkoa umepokea kiasi cha Tshs 3,380,560,000.00 Kumekuwa na ongezeko la bajeti ya dawa kwa kiasi Tshs 400,000,000.00 sawa na asilimia 11.8. Hadi kufikia mwezi Juni 2025 wastani wa upatikanaji wa dawa ni asilimia 94.
"Katika sekta ya miundombinu, barabara kuu ya kutoka Mpanda–Tabora, Mpanda–Vikonge na Mpanda–Sitalike zimekamilika na zinatumika, huku nyingine kama Vikonge–Luhafwe na Kibaoni–Sitalike zikiendelea kujengwa. Daraja kubwa la Kavuu linaendelea kujengwa na lile la Msadya tayari limekamilika."Amesema Mhe.Mwanamvua.
Mhe,Mwanamvua amesema Sekta ya elimu imenufaika ambapo shule mpya 129 zimejengwa kupitia programu mbalimbali za Serikali ikiwemo BOOST, UVIKO na SEQUIP. Shule ya wavulana ya kanda imepokea zaidi ya shilingi bilioni 4, sawa na shule maalumu ya wasichana katika Halmashauri ya Nsimbo.


