Na Avelina Musa - Dodoma.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ametoa wito kwa vituo vyote vinavyotoa huduma za afya nchini viweke wazi mikataba ya utoaji wa huduma bora kwa mteja ili kuepuka migogoro na migongano baina ya watoa huduma na wateja.
Mhe. Mhagama amesema hayo Leo June 25 mwaka huu wakati akizindua Mkataba wa Huduma kwa Mteja Jijini Dodoma,ambapo amesema mkataba huo ni ahadi baina ya Wizara ya Afya na Wananchi na unalenga kutoa huduma bora,sahihi na kwa wakati ili kuleta mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma za afya hatua ambayo itaongeza uwajibikaji kwa watendaji wa sekta hiyo.
Mhe.Mhagama ameagiza vituo vyote vinavyotoa huduma za afya vizingatie matumizi ya mifumo iliyowekwa kuhusiana na utoaji wa huduma za afya nchini ili kupunguza malalamiko yasiyo ya msingi.
"Inakuwaje mgonjwa anaporuhusiwa ama kinapotokea kifo kituo cha kutolea huduma kinasema tunakudai, mgonjwa yeye anadai kwamba ameshalipa jambo gani limejificha na limejificha wapi? Tunataka watu wawe na mikataba na kila jambo liwe wazi ili tukiweza kutengeneza uwazi tutawabaini wale ambao hawana uwezo."Amesema Mhagama.
"Na nyie mmeona wakati mwingine kumekuwa na ugumu wa kutekeleza miongozo inayohusiana na huduma za hifadhi ya maiti,inabaki kuwa kelele maiti inashikiliwa eti inadaiwa,na ndio maana niliwaambia sasa maiti huyo kama alikuwa anajilipia mwenyewe matokeo yake ni nini? Tunataka afufuke ndo aende kujilipia?" Amesema Mhagama.
Aidha amesema huduma ambazo zimetajwa kwenye mkataba huo zinaendana na sera na miongozo mbalimbali ya uendeshaji wa shughuli za afya nchini,ushauri wa kitaalamu kuhusu uendeshaji wa shughuli za afya,maswala ya chanjo,vyeti vya usajili wa kitaaluma,leseni za kitaaluma,vibali mbalimbali,taarifa za sekta ya afya,mikataba ya kimataifa waliyoingia nayo,mikataba ya ndani na huduma nyinginezo.
Waziri Mhagama amesema kupitia Mkataba huo wa huduma Bora kwa mteja Wizara ya Afya imejipanga Vizuri kuyatekeleza hayo kwa ubora unaotakiwa.