Na Avelina Musa - Dodoma.
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde leo amekabidhi jengo la kupumzikia wananchi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ambalo litasaidia kutatua changamoto ya wananchi wengi ambao hawakuwa na eneo lenye staha la kupumzika wakati wakiwa wanawahudumia wagonjwa wao.
Hafla hiyo ya kukabidhi jengo hilo limeongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule leo tarehe 25.06.2025 ambapo amesema Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya maboresho ya vifaa na huduma ya Afya kwenye Hospitali hii ya Rufaa Dodoma.
Mhe.Senyamule amesema kazi iliyofanywa na Mbunge Mavunde ni ya kuigwa mfano kwa kuwa ameunga mkono jitihada za Mh. Rais kwenye maboresho ya huduma za Afya.
"Jengo hili litasaidia sana kuwafanya wananchi wa Dodoma na nje ya Dodoma kukaa kwenye mazingira mazuri na nadhifu,hivyo naagiza jengo hili kutunzwa na kusimamiwa vyema kwa lengo lililokusudiwa"Amesema Senyamule.
"Nakupongeza Mbunge Mavunde kwa kuanzisha ujenzi wa uzio wa Hospital ya Rufaa,nitoe rai kwa wadau wengine kuunga mkono jitihada hizi kubwa za Mbunge katika kuweka uzio wa Hospitali ya Rufaa”Amesema Senyamule.
Akitoa taarifa ya awali,Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Dkt. Ernest Ibenzi amesema Hospitali hiyo hivi sasa inaendelea na upanuzi mkubwa na ujenzi wa majengo mapya ya kutoa huduma kwa wananchi na hivyo kutumia nafasi hiyo kumshukuru Mbunge Mavunde kwa ushirikiano mkubwa ambao amekuwa akiutoa kwenye Hospitali ikiwemo ya ujenzi wa jengo la wananchk na hatua ya kuanzisha ujenzi wa uzio wa Hospitali hiyo.
Aidha,akizungumza katika hafla hiyo Mbunge Anthony Mavunde amesema ujenzi wa jengo hilo umechochewa na idadi kubwa ya wananchi ambao wanafika Hospitalini hapo kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wao na kukosa maeneo ya kupumzika hasa nyakati za usiku.
Hata hivyo wananchi walioshiriki katika Uzinduzi huo wamemshukuru Mbunge Mavunde kwa kazi nzuri aliyoifanya na anayoendelea kuifanya katika Jiji la Dodoma.
Mwisho.