Mbali na ziara hiyo, Rais Dkt. Samia amepokea mwaliko maalum wa kufanya ziara ya kikazi Msumbiji na Visiwa vya Comoro, lengo likiwa ni kuimarisha uhusiano wa kimataifa na ushirikiano wa maendeleo.
Wizara ya Fedha na Wizara ya Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji zinatarajiwa kuwasilisha bajeti kuu ya serikali pamoja na hali ya uchumi, ikiwa kwa mara ya kwanza bajeti hiyo inahudumiwa kwa fedha za ndani. Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma Leo Juni 11 2025 alieza kuwa bajeti hii ni ya kihistoria na inalenga kutoa mwelekeo wa uchaguzi wa mwaka 2025.
Msigwa alihimiza wananchi kufuatilia kwa karibu bajeti hiyo, akisema kuwa ni fursa ya kushuhudia maendeleo makubwa yaliyofikiwa na serikali ya Awamu ya Sita. "Hii ni bajeti ya mwisho ya serikali ya Awamu ya Sita, na asilimia kubwa ya fedha zinatokana na mapato ya ndani," alisisitiza.
Kwa mara ya kwanza, Tanzania imepokea gawio la shilingi trilioni 1.28 kutoka mashirika ya umma, hatua iliyochagizwa na sera za 4R zilizoasisiwa na Rais Dkt. Samia. Uwekezaji wa kina wa serikali umefikia shilingi trilioni 86, na matarajio ni kwamba gawio hili litaendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.
Awamu ya Pili ya ujenzi wa mji wa serikali imefikia asilimia 90.1, ikihusisha majengo 34 ambapo sita tayari yanatumika. Mradi huu umegharimu shilingi bilioni 738.9, na miundombinu ya kisasa, ikiwa ni pamoja na barabara za lami zenye urefu wa kilometa 59.1, umeme wa chini ya ardhi wa kilometa 42, na upandaji wa miti 233,000, inaimarisha mazingira ya mji huo.
Msigwa aliwaasa vijana, hasa wa vyuo vikuu, kutumia mitandao ya kijamii kwa njia chanya. Alisisitiza kuwa matumizi mabaya ya mitandao yanaweza kuwa kikwazo kwa maendeleo, na sheria zitaendelea kutekelezwa kwa wale wanaovunja sheria.