Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mhe. Antonio Guterres yaliyofanyika kando ya Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari unaofanyika Jijini Nice nchini Ufaransa leo tarehe 10 Juni 2025.
Mazungumzo hayo yamelenga kuimarisha zaidi ushirikiano baina ya Tanzania na Umoja wa Mataifa kupitia Taasisi mbalimbali zilizo chini ya Umoja wa Mataifa.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri na Mazingira na Hali ya Hewa wa Sweden Mhe. Romina Pourmokhtari.
Mazungumzo hayo yamelenga kuongeza ushirikiano baina ya Tanzania na Sweden katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kubadilishana maarifa katika kilimo janja, kuhamisha teknolojia za kisasa za kulinda mazingira pamoja na matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Makamu wa Rais yupo nchini Ufaransa kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Tatu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari unaofanyika katika Mji wa Nice.