Na Avelina Musa - Dodoma.
Taasisi ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imeshiriki wiki ya Utumishi wa Umma ambapo mpaka sasa imewahudumia zaidi ya wagonjwa 70 katika banda lao lililopo kwenye Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Hayo yamesemwa na Daktari bingwa wa upasuaji mifupa Moi Dkt. Tumaini Minja wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema wagonjwa wengi waliowahudumia ni wenye matatizo ya maumivu sugu ya mgongo, magoti, nyonga na mishipa ya fahamu ambapo baadhi ni wagonjwa waliowahi kutibiwa MOI na wengine ni wapya.
"Waliopata huduma kwa mara ya kwanza wengine wenyeji wa Dodoma na wanaotokea pembezoni"Amesema Dkt.Minja.
“Wagonjwa wengi wanaotufikia ni wa umri kati ya miaka 45 hadi 60, na matatizo yao yanatokana zaidi na changamoto za umri, uzito mkubwa kupita kiasi, pamoja na mitindo ya maisha isiyojumuisha mazoezi ya mwili,” alisema Dkt. Minja.
Amesema magonjwa hayo yanatibika kulingana na hali ya mgonjwa, ambapo wengine huhitaji upasuaji na wengine hutibiwa kwa kutumia dawa au njia mbadala zisizo za upasuaji.
Dkt. Minja amesema huduma zinazotolewa kwenye maonesho hayo ni uchunguzi wa awali, ushauri wa kitabibu na upangaji wa rufaa kwa matibabu zaidi MOI.
Aidha amesema MOI imejipanga kutoa huduma mahsusi kwa wanamichezo, kwani wengi wao hukumbwa na majeraha ya magoti, enka na viungo mbalimbali kutokana na shughuli zao.
“Tunawahamasisha wanamichezo wote kutembelea banda letu hapa Chinangali kwa ajili ya uchunguzi wa awali na kupata ushauri wa kiafya kabla ya majeraha kuwa makubwa. Matibabu si lazima yaanze baada ya maumivu, kinga ni bora zaidi,” amesema Dkt.Minja.
Hata hivyo Dkt.Minja amewakaribisha wakazi wa Dodoma na mikoa jirani kutembelea Banda la MOI ili waweze kupata huduma stahiki.
Mwisho