Na Avelina Musa - Dodoma.
Waziri wa Ujenzi, Mhe,Abdallah Ulega ameliomba Bunge kuridhia na kupitisha bajeti ya Wizara ya ujenzi kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kiasi cha shilingi trilioni 2.28 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Miradi ya Maendeleo.
Akiwasilisha bungeni bajeti ya wizara yake ambayo imeahidi ujenzi zaidi wa barabara na madaraja nchini huku akisisitiza uchapakazi zaidi na utu kwenye utekelezaji wa miradi.
Akizungumza bungeni Jijini Dodoma, Mhe Ulega amesema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika eneo la ujenzi kwenye miaka ya karibuni, kazi kubwa itaendelea kufanyika ili kuhakikisha maeneo yote ya nchi yanafikika katika majira yote ya mwaka.
“Mheshimiwa Spika, tumepiga hatua kubwa katika ujenzi wa barabara na madaraja. Hata hivyo, bado kuna changamoto ya baadhi ya maeneo kutofikika kwa barabara na mengine yasiyofikika katika majira fulani ya mwaka.
“Katika bajeti hii niliyoiwasilisha leo, ninaomba kuahidi Bunge lako kwamba serikali itaendelea kujenga barabara na madaraja ili kuongeza maendeleo ya taifa letu lakini pia kufanya wananchi wetu waishi maisha ya utu,” amesema Ulega.
Mhe,Ulega ametaja baadhi ya vipaumbele vya kimkakati katika bajeti ya mwaka 2025/2026 ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara na madaraja kwenye maeneo zaidi nchini, kupunguza foleni na misongamano, uwezeshaji makandarasi wazawa, ufungaji taa za barabarani na matumizi ya teknolojia kwenye mizani ili kupunguza usumbufu na rushwa.
“ Tuna mipango yetu na vipaumbele vyetu kama Taifa lakini tunaangalia pia utu wa watu wetu. Utu kwa maana kwamba athari kwenye miundombinu zisifanye watu waishi kama si binadamu,” alisema.
Katika eneo la uwezeshaji makandarasi wazawa, Ulega amesema serikali imeongeza ukomo wa miradi ya ujenzi wanayotakiwa kupewa makandarasi wa ndani kutoka shilingi bilioni 10 hadi shilingi bilioni 50.
“ Kuanzia sasa, makandarasi wa ndani watapewa kipaumbele kwenye miradi yote ya ujenzi ambayo thamani yake haizidi shilingi bilioni 50. Tuna matumaini kwamba hali hii itaongeza mzunguko wa fedha ndani ya nchi lakini pia uwezo wao wa kujenga miradi mikubwa,” amesema.